Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Mei 27, 2024 Local time: 11:59

Waandamanaji waitaka Ufaransa iondoke Chad


Waandamanaji mjini N'Djamena wakitia moto bendera ya Ufaransa wakati wa maandamano kupinga taifa hilo mtawala wa zamani wa kikoloni
Waandamanaji mjini N'Djamena wakitia moto bendera ya Ufaransa wakati wa maandamano kupinga taifa hilo mtawala wa zamani wa kikoloni

Polisi wa Chad wametumia mabomu ya kutoa machozi na mabomba ya maji kuwatawanya mamia ya waandamanaji waliokuwa wanapinga kuwepo kwa Ufaransa nchini mwao.

“Ufaransa ondoka,” “Hatutaki ukoloni,” ni matamshi yaliyokuwa yanatolewa na mamia ya waandamanaji katika mji mkuu wa Chad N’Djamena siku ya Jumamosi.

Waandamanaji hao wanadai kwamba taifa hilo la zamani la kikoloni wanaliunga mkono Baraza la Kijeshi linalotawala nchini humo kwa hivi sasa.

Polisi wanasema walilazimika kuingilia kati na kuwatawanya waandamanaji walipoanza kushambulia vituo vya mafuta vya kampuni ya Total, ambayo ni alama kubwa ya Ufaransa, na kuharibu pampu za kutia mafuta na kuharibu baadhi ya bidhaa kutoka Ufaransa.

Maandamano haya yaliyoitishwa na muungano wa upinzani wa mashirika ya kiraia Wakit Tamma yaliidhinishwa na maafisa wa usalama, na awali kulikuwepo na idadi kubwa ya polisi waliowazunguka na kuwaruhusu waandamanaji kuandamana kati kati ya mji mkuu.

Wakati wa maandamano ya Jumamosi wanafunzi wa shule za sekondari na vyuo vikuu walipita kwa pikipiki na kuunga mkono waandamanaji wakiimba wafaransa waondoke.

Idriss Moussa mwalimu wa shule ya sekondari ameliambia shirika la habari la Ufaransa AFP kwamba “ikiwa tunaendelea kukabiliwa na matatizo hii leo, hii ni kwa sababu ya makosa ya Ufaransa, inayotuzuia kuchukua maamuzi yetu kwa njia ya uhuru.”

Maandamano haya yanafanyika wiki mbili baada ya kiongozi wa baraza la kijeshi Mahamet Deby, kutangaza kwamba mazungumzo ya kitaifa yaliyopangwa kufanyika Mei 10 yameakhirishwa kwa muda usiojulikana.

XS
SM
MD
LG