Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Julai 25, 2024 Local time: 16:43

Waafrika wakosoa mahakama ya ICC


Mwendesha mashtaka Fatou Bensouda wa mahakama ya ICC
Mwendesha mashtaka Fatou Bensouda wa mahakama ya ICC
Waziri wa sheria wa Rwanda anasema mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita ICC hulenga kundi fulani kwa misingi ya ubaguzi katika utendaji kazi zake. Matamshi yake yalitolewa wakati mahakama hiyo ikiadhimisha ya miaka 15 tangu ilipobuniwa. Alisema hivi leo Waafrika wengi wanajiuliza ikiwa bara la Afrika lina haja tena na mahakama hiyo ya ICC.

Mnamo Julai 17 mwaka wa 1998 wajumbe katika mkutano wa kimataifa mjini Roma walipiga kura kubuni mahakama hiyo kama hatua ya mwisho ya kulinda haki kwa kushtaki na kusikiliza kesi za watuhumiwa wa mauaji ya halaiki, uhalifu wa kivita na uhalifu mwingine ambao mahakama za vyombo vya dola zinashindwa kukabiliana nayo au hazina uwezo wa kuchukulia hatua za kisheria.

Kwa sasa mahakama hiyo ya kimataifa yenye makao yake The Hague, ina kesi zinazohusu nchi 8 za Afrika ikiwemo Kenya, Sudan na Ivory Coast.
Rwanda ni mojawapo ya nchi zilizokataa kutia saini mkataba huo wa Roma na ni mkosoaji mkubwa wa mahakama hiyo ya ICC.

Waziri wa sheria wa Rwanda Johnston Busingye aliiambia sauti ya Amerika kwamba hata ingawa Rwanda inaunga mkono dhana ya sheria za kimataifa, anahisi kwamba mahakama ya ICC inawalenga Waafrika pasipo haki.

Kote barani Afrika, uungaji mkono wa mahakama ya ICC unafifia. Mnamo mwezi Mei Umoja wa Afrika ulipiga kura kurejesha kesi dhidi ya rais wa Kenya na naibu rais nchini Kenya kutoka ICC. Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika, waziri mkuu wa Ethiopia Hailemariam Desalegn aliishtumu ICC kwa ubaguzi wa rangi. Mahakama hiyo inakanusha kuwa inawalenga Waafrika.

Na katika kura ya maoni iliyofanywa na wananchi wa Kenya, asili mia 39 walisema wanaunga mkono kesi dhidi ya rais wao na naibu wake kusikilizwa na ICC, lakini asili mia kubwa zaidi ya wakenya wanataka kesi hizo zirejeshwa nchini Kenya au zifutwe kabisa.

Rais wa Kenya bw. Uhuru Kenyatta na Naibu rais bw. William Ruto wameongoza kampeni kali dhidi ya ICC. Lakini mahakama hiyo inasema kesi dhidi yao zitaanza baadaye mwaka huu.
XS
SM
MD
LG