Taasisi ya kitaifa ya jiografia imesema kwamba jivu lilipaa angani kwa urefu wa takriban kilomita nne na nusu kabla ya kutawanywa na upepo mkali kwenye maeneo ya karibu, ikiwemo miji. Mlipuko huo umekuwa kivutio kikubwa cha watalii wakati leo Jumatatu ikiwa siku ya kusherehekea watakatifu nchini humo.
Kisiwa cha La Palma ni sehemu ya visiwa vya Canary. Lava kutoka kwenye volcano hiyo kuelekea kwenye bahari ya Atlantic inasemekana kufunika takriban ekari 2,400 tangu Septemba 19 ilipoanza, kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa huduma ya satellite ya Umoja wa Ulaya.
Tayari zaidi ya watu 7,000 wamelazimika kuhama makwao huku zaidi ya nyumba 2,000 zikiharibuwa na lava kutoka kwenye volcano hiyo. Hata hivyo mamlaka husika zimesema kwamba hakuna majeruhi walioripotiwa kufikia sasa. Wataalam wanasema kwamba ni vigumu kutabiri ni lini hali hiyo itamalizika kwa kuwa mambo mengi yanafanyikia chini ya ardhi.