Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Machi 28, 2024 Local time: 23:53

Mawaziri wa Afrika na Ulaya wajadili usalama Mali


Waziri wa mambo ya nje wa Mali Tieman Hubert Coulibaly akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari.
Waziri wa mambo ya nje wa Mali Tieman Hubert Coulibaly akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari.
Wakati vikosi vya Chad vinasaidia kudhibiti mji muhimu ulioko jangwani, huko Mali, wawakilishi wa mataifa ya Kiafrika na ya Ulaya walikutana mjini Brussels Jumanne kujadili uwezekano wa kubuni kikosi cha kimataifa kusaidia kudhibiti taifa hilo la Afrika Magharibi.

Wawakilishi hao walisema uamuzi wowote wa kugeuza kikosi cha nchi za Afrika magharibi kuwa kikosi cha kimataifa cha kuleta uthabiti nchini Mali, lazima kipitishwe na Umoja Mataifa na serikali ya Mali.

Desire Ouedraogo, ambaye anaongoza tume ya jumuiya ya kiuchumi ya nchi za Afrika magharibi ECOWAS, alisema matatizo ya Mali sio suala tu la usalama wa kitaifa au wa kikanda, lakini ni suala la usalama wa kimataifa. Alisema jumuiya ya kimataifa lazima ihakikishe kuwa Mali kaskazini haitumiwi kuwa hifadhi ya magaidi na walanguzi wa madawa haramu.

Matamshi yake yalifuatia mazungumzo miongoni mwa wawakilishi wa mataifa ya jumuiya ya Ulaya, Afrika na Umoja Mataifa, juu ya jinsi ya kuratibu juhudi za kuleta uthabiti huko Mali, baada ya wanamgambo wa kiislamu kuzusha mzozo wa kisiasa. Serikali ya Mali imeahidi kufuata masharti ikiwa ni pamoja na kufanya uchaguzi wa kidemokrasia.

Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa ulaya Catherine Ashton, alisema ulaya tayari inatimiza ahadi yake ya kusaidia kulipatia mafunzo jeshi la Mali, na imetenga zaidi ya dola millioni mia 4 za msaada kwa mwaka huu kusaidia taifa hilo la Afrika magharibi.

Hadi sasa, Ufaransa imekuwa nchi pekee ya Ulaya kupeleka wanajeshi huko Mali. Mashambulizi ya vikosi vya Ufaransa yaliyofanikiwa kuwarudisha nyuma wanamgambo wa kiislamu, yamepongezwa sio tu kutoka kwa waafrika, lakini viongozi wa nchi za magharibi kadhalika, ikiwa ni pamoja na makam rais wa Marekani Joe Biden, ambaye alikutana na rais wa Ufaransa Francois Hollande Jumatatu huko mjini Paris.
XS
SM
MD
LG