Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Mei 27, 2024 Local time: 07:33

Vijana 24 wafikishwa mahakamani Mombasa


Ghasia zazuka mjini Mombasa baada ya kifo cha Imam Rogo
Ghasia zazuka mjini Mombasa baada ya kifo cha Imam Rogo

Kaimu waziri wa usalama wa ndani Yusuf Haji amekiri ghasia zilizotokana na mauaji zimekuwa kubwa kuliko makadirio ya serikali, ulinzi umeongezwa

Vijana 24 walifunguliwa mashtaka mjini Mombasa Jumatano kwa kuhusika katika ghasia zilizozuka kufuatia mauaji ya mhubiri maarufu wa ki-Islam nchini Kenya, Imam Aboud Rogo Mohamed.

Rogo ambaye anashutumiwa kuwa gaidi kwa kuhubiri jihad au vita vitakatifu alikuwa mtu mwenye ushawishi na mashuhuri katika jamii ya waislam akiungwa mkono wa wanaharakati mjini Mombasa, Lamu na Kilifi. Mauaji yake yamechochea wimbi la ghasia lililosababisha uharibifu mkubwa wa mali za watu binafsi na majengo ya serikali pamoja na kuchomwa moto makanisa matatu mjini Mombasa.

Watu hao 24 wamefunguliwa mashtaka ya uhalifu wa kukutana kinyume cha sheria na kushiriki katika ghasia Jumanne na wataendelea kuwepo kizuizini hadi Septemba 3 wakati maombi yao ya kuachiliwa kwa dhamana yatakapoamuliwa.

Kwingineko kaimu waziri wa usalama wa ndani Yusuf Haji amekiri kwamba ghasia zilizotokana na mauaji zimekuwa kubwa kuliko makadirio ya serikali lakini alidai usalama umeongezwa ili kuepusha ghasia zaidi, wizi wa mali na uhalifu mwingine wa makusudi ambao umepelekea kudumaza uchumi wa mji huo wa pwani.

“Hatukutegemea jambo hili kufikia kiwango hiki”, alisema Haji akielezea ghasia ambazo zimepelekea raia kukatwa na mapanga hadi kufa zilizofanywa na wafuasi wanamgambo wa Rogo katika mji wa Mombasa Jumatatu.

Wakati akizungumza kwenye makao makuu ya jeshi la majini la Kenya huko Mtongwe, polisi walikuwa wanafanya msako wa nyumba moja hadi nyingine katika vitongoji vya Kisauni na mtaa wa Majengo ambako ni kiini cha ghasia. Maafisa wa polisi waliwakamata vijana wanane walioshukiwa kuhusika na ukataji watu mapanga na kuchoma moto majengo katika ngome ya wanaharakati.
XS
SM
MD
LG