Hamas na serikali ya Israel wamekataa pendekezo la viongozi wa Palestina katika ukingo wa magharibi la kusitisha mapigano kwa siku moja, huku mashambulio ya Israel ya anga na nchi kavu yanasababisha uharibifu mkubwa zaidi kwa kulenga shabaha maeneo muhimu ya wanamgambo wa Hamas.
Siku ya Jumatatu usiku katika mapigano makali ya Israel kuwahi kutokea tangu kuanza mapigano ya Gaza wiki tatu zilizopita jeshi la Israel limeharibu kituo muhimu cha kuzalisha umeme, pamoja na kuharibu kabisa nyumba ya ofisa mkuu wa Hamas na kituo chao cha matangazo.
Maafisa wa afya wa Palestina wanasema mashambulizi hayo ya Jumatatu pekee yamesababisha vifo vya watu wasiopungua 26 katika ukanda wa Gaza, huku jeshi likiendelea na kampeni ambayo Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu alionya itaweza kuendelea kwa muda mrefu.
Maafisa hao wanasema idadi ya vifo kwa jumla imefikia watu 1,100 ilipofika Jumanne, wengi wao wakiwa raia na watoto, pamoja na kuharibiwa nyumba nyingi za raia.
Shambulizi moja la anga Jumanne lililenga malori ya mafuta kwenye kituo pekee cha umeme huko Gaza na kusababisha kufungwa. Kabla ya shambulizi hilo, tayari uharibifu kwenye mfumo wa umeme ulisababisha kupunguzwa huduma za umeme na kupelekea huduma hiyo kutolewa kwa saa nne kwa siku.
Bwana Netanyahu aliwaambia wa-Israel katika hotuba kwa njia ya televisheni Jumatatu kwamba wajiandae kwa kampeni ndefu ya mapambano dhidi ya kundi la Hamas.