Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumapili, Novemba 03, 2024 Local time: 16:47

Uswisi yaendelea kuchunguza rushwa ndani ya FIFA


Viongozi ndani ya FIFA
Viongozi ndani ya FIFA

Waendesha mashtaka wa Uswisi wanachunguza matukio 53 ya uwezekano wa kuhalalisha fedha zilizopatikana kinyume cha sharia yanayohusisha utaratibu wa FIFA kugombania nafasi ya kuandaa michuano ya kombe la Dunia kwa mwaka 2018 na 2022.

Mwanasheria mkuu wa Uswisi, Michael Lauber alisema jumatano kwamba kuingiza na kutoka kwa fedha hizo kuliripotiwa na mabenki kupitia mfumo wa Uswisi wa kutoa onyo la mapema la kupambana na fedha za ulanguzi . Alisema mabenki yalifanya kazi yao kwa kuripoti harakati hizo na walionya kwamba kesi hiyo ni “kubwa na ni ya kutatanisha”.

Mwanasheria mkuu wa Uswisi, Michael Lauber
Mwanasheria mkuu wa Uswisi, Michael Lauber

Lauber aliwaambia waandishi wa habari kwamba kuna uwezekano pia wa kumhoji rais wa FIFA, Sepp Blatter ambaye amekubali kujiuzulu kufuatia sakata la rushwa lililowahusisha viongozi kadhaa wa shirikisho hilo la kandanda duniani .

Uchunguzi wa Uswisi umekuwa ukiangalia shutuma za usimamizi mbaya wa fedha na kuhalalisha fedha zinazopatikana kinyume cha sheria kuhusiana na kuichagua Russia na Qatar kuandaa michuano ya kombe la Dunia mwaka 2018 na 2022.

Mashtaka tofauti yaliyotolewa na Marekani mwezi uliopita dhidi ya maafisa tisa wa FIFA na wakurugenzi watano wa mashirika ya biashara kwa makosa kadhaa ikiwemo uhalifu wa biashara na kuhalalisha fedha haramu.

FIFA imeakhirisha utaratibu wa mchakato wa kumpata mwenyeji wa kombe la Dunia mwaka 2026 kwa sababu ya kashfa inayoendelea hivi sasa.

Mwenyeji wa michuano ya mwaka 2026 alipangwa kuchaguliwa na wanachama wa FIFA katika mkutano wa mwaka 2017 huko Malaysia. haijulikani wazi lini uamuzi huo utafanyika tena.

Hati za mahakama ya Marekani zilizotolewa hadharani mwanzoni mwa mwezi huu zinaonesha kwamba mjumbe wa zamani wa kamati kuu ya FIFA, Mmarekani Charles Blazer, amekiri kupokea hongo kuhusiana na Kombe la Dunia 1998 na 2010.

XS
SM
MD
LG