Wapelelezi wa haki za binadamu wamegundua hati za kisiri nchini Libya zinazoonyesha ushirikiano wa karibu baina ya taasisi za kijasusi za nchi za Magharibi na utawala wa zamani wa Libya, huku idara ya kijasusi ya Marekani CIA ikisaidia serikali ya Moammar Ghadafi kuwateka nyara watuhumiwa wa ugaidi kutoka nchi za kigeni. Watafiti wa haki za binadamu waligundua hati hizo jana Ijumaa mjini Tripoli katika ofisi moja iliyokuwa inatumiwa na mkuu wa kijasusi wa Libya. Moussa Koussa, mshirika wa karibu wa Ghadafi, aliongoza idara ya kijasusi ya Libya kati ya mwaka wa 2003 na 2004 na baadaye kufanya kazi kama waziri wa mambo ya nje wa Libya. Taarifa za hivi karibuni juu ya shughuli za idara ya kijasusi ya Marekani, zinazonyesha kuwa Libya ilikuwa inahusika katika mpango wa idara hiyo wa kuwazuilia , kuwahamisha na hata kuwasaili watuhumiwa wa ugaidi katika nchi za nje.
Idara ya Kijasusi ya Marekani yatajwa kushirikiana na utawala wa Ghadafi zamani