Idara ya Maendeleo ya Kimataifa ya Marekani-USAID, itatoa zaidi ya dola milioni 120, kwa ajili ya program za lishe na kupunguza ukame nchini Ethiopia.
Mkurugenzi wa USAID, Raj Shah, anasema mpango huo utawanufaisha watu milioni 1.5. Shah anaongoza ujumbe kuelekea Kenya na Ethiopia kuonesha uungaji mkono kwa eneo lililokumbwa na baa la njaa na ukame.
Ujumbe huo utajadili maendeleo katika eneo hilo pamoja na vikwazo vinavyozuia mashirika ya misaada ya kibinadamu kuwasaidia waathirika wa njaa nchini Somalia na wale waliopo kwenye kambi nchini Kenya na Ethiopia.
Pembe ya Afrika inakumbwa na ukame sugu ambao umesababisha takribani watu milioni 13 wakihitaji msaada wa chakula cha kutosha, maji na huduma za afya.
Umoja wa Mataifa unakadiria maelfu ya watu wamekufa katika eneo hilo na unasema watu 750,000 wapo hatarini kufa katika kipindi cha miezi michache ijayo.
Uhaba wa chakula unatarajiwa kuendelea angalau kwa miezi miwili mingine, hadi msimu ujao wa mavuno.
Maelfu ya wasomali wamekimbia nyumba zao wakitafuta chakula na maji, wakihamia kwenye kambi za wakimbizi katika maeneo ya Mogadishu au nchi jirani za Kenya na Ethiopia.
Sehemu kubwa ya kusini na kati kati ya Somalia ipo chini ya udhibiti wa wanamgambo wa al-Shabab, ambao wanapigana kuiangusha serikali dhaifu ya muda ili waweke sheria kali ya ki-Islam. Kundi hilo limezuia makundi mengi ya misaada kuendesha shughuli zake kwa uhuru katika maeneo yaliyo chini ya udhibiti wao.
USAID kusaidia Ethiopia na dola milioni 120

Idara ya maendeleo ya kimataifa ya Marekani itatoa dola milioni 120 kwa Ethiopia kwa ajili ya program za lishe na kupunguza ukame