Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Aprili 20, 2024 Local time: 20:14

Marekani yasitisha $ milioni 350 kwa Malawi


Waandamanaji wakichoma mimea katika mtaa mmoja huko Lilongwe nchini Malawi, Julai 20,2011
Waandamanaji wakichoma mimea katika mtaa mmoja huko Lilongwe nchini Malawi, Julai 20,2011

Marekani imesitisha msaada wa dola milioni 350 kwa Malawi, kufuatia mapambano kati ya polisi na waandamanaji katika nchi hiyo iliyo kusini ya Afrika.

Idara ya serikali ya Marekani ya The Millennium Challenge Corporation, ambayo inasaidia nchi zinazoendelea imesema leo kwamba itatathmini ushirika wake na Malawi.

Idara hiyo imeelezea wasi wasi kuhusu majeshi ya serikali kutumia nguvu na kuvidhibiti vyombo vya habari vilivyokuwa vikiripoti juu ya maandamano hayo. Idara hiyo inasema hali hiyo inaleta mashaka juu ya kujitolea kwa Malawi kuzingatia utawala bora. Watu wasiopungua 18 waliuwawa Jumatano na Alhamisi wiki iliyopita wakati polisi walipopambana na waandamanaji mitaani katika miji mitatu ya Malawi.

Maafisa walisema watu 100 walifikishwa katika mahakama za Malawi Jumanne kukabiliana na mashtaka yanayohusiana na maandamano.

Msemaji wa polisi John Namalenga alisema washukiwa wanakabiliwa na mashtaka tofauti ikiwemo uchomaji moto, wizi wa ngawira na wizi wa mali.

Idara ya Millenium Challenge Corporation imeundwa kusaidia nchi zinazoendelea ambazo zinalinda haki za binadamu na kuzingatia utawala wa kisheria.

Waandamanaji nchini Malawi walikuwa wanapinga uhaba wa mafuta, kuongezeka kwa bei za bidhaa na kile wanachosema kupuuza haki za kiraia.

XS
SM
MD
LG