Waziri mdogo wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani Johnnie Carson anasema majeshi zaidi yanahitajika nchini Somalia ambako wanamgambo wa kiislamu wenye msimamo mkali wanajaribu kuiangusha serikali ya mpito ya nchi hiyo.
Carson alitoa matamshi hayo Jumatatu nje ya mkutano wa viongozi wa Umoja wa Afrika wanaokutana katika mji mkuu wa Uganda, Kampala.
Mkutano huo Jumatatu ulijadili mabadiliko ya amri ya walinzi wa amani wa Umoja wa Afrika walioko Somalia ambayo yanasaidia kulinda maeneo muhimu ya serikali. Taarifa ya baadaye ilisema AU itaadhinisha mabadiliko ya amri hiyo ikiwa na maana kuwa huenda walinzi wa amani wakaruhusiwa kupambana na waasi nchini Somalia. Amri ya sasa ya majeshi hayo ya AU ni kulinda usalama na kufanya mashambulizi pale tu yanapolazimika kujitetea.
Jeshi la AU huko Somalia hivi sasa lina kiasi cha wanajeshi elfu sita tu kutoka Uganda na Burundi.
Wanadiplomasia wa Afrika wanasema juhudi za kufikia maamuzi madhubuti kwa taifa la Somalia, katika mkutano huo wa Umoja wa Afrika, zinapingwa na wajumbe kutoka Eritrea. Eritrea ni nchi pekee ya pembe ya Afrika, ambayo si mwanachama wa shirika la kiuchumi la eneo hilo IGAD, inayopinga mipango ya nchi jirani kama vile Ethiopia, Kenya na Uganda, kuimarisha kikosi cha AMISOM na kuboresha mikakati kuwezesha makamanda wake kuwa na mamlaka ya kukabiliana na mashambulizi ya Al Shabab.