Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Aprili 19, 2024 Local time: 01:48

Miungano ya vyama vya kisiasa yatawala uchaguzi wa rais


Waziri Mkuu, Raila Odinga na Makamu Rais, Kalonzo Musyoka wakiwasili kwenye viwanja vya Uhuru Park mjini Nairobi kwa mkutano wa hadhara.
Waziri Mkuu, Raila Odinga na Makamu Rais, Kalonzo Musyoka wakiwasili kwenye viwanja vya Uhuru Park mjini Nairobi kwa mkutano wa hadhara.

Miungano ya vyama vya kisiasa katika uchaguzi wa urais hapo march nne ndiyo imetawala , kutokana na kile ambacho kinaelezewa kuwa katiba mpya ya kenya imeweka masharti katika kipengele cha kuwania urais na hivyo kuwalazimisha wagombea wengi wa nafasi hiyo ya juu ya uongozi kubuni njia za kuweza kujipatia ushindi kwa kuunganisha nguvu za vyama vyao vya kisiasa.

Tukitupia jicho nini kimechangia kuwepo na sharti hilo katika katiba mpya ya kenya, ni vyema tuelewe kuwa kenya ni nchi yenye makabila 40 yanayozungumza lugha mbalimbali za kienyeji ambayo pia yanaishi katika maeneo mbalimbali ya taifa hilo na kufuata tamaduni tofauti. Ingawa kutokana na elimu na nafasi za ajira kuna maeneo ambayo makabila ya Kenya yamechanganyika, suala la ukabila bado ni sugu. Wengi wanatambuliwa kwa majina yao na kukubaliwa au kubaguliwa kutokana na makabila yao.

Lakini kinachowaunganisha wakenya ni lugha ya Kiswahili ambayo ni lugha ya taifa na pia ni lugha rasmi. Wakenya pia hutumia Kiingereza kama lugha rasmi ya mawasiliano.
Lakini kwa miaka nenda miaka rudi ,Kenya imesumbuliwa na tatizo la ukabila. Tatizo hili ni dhahiri pia linapokuja suala la vitambulisho vya kitaifa na hata wakati wa uchaguzi, suala la ukabila limekuwa likizungumziwa sana.

Lakini hali inaanza kubadilika na uchaguzi mkuu ujao utakuwa mtihani wa kwanza mkubwa wa kuyeyusha uhasama wa kikabila nchini humo. Kutokana na katiba mpya na sheria mpya za uchaguzi, inambidi mshindi wa kiti cha rais kushinda uchaguzi kwa kupata asili mia 51 ya kura, pamoja na kupata wingi wa kura katika nusu ya county 47 za Kenya. Hili linawezekana tu kwa kuunda ushirika wa kisiasa na watu wa makabila mbalimbali ili kuzoa kura kwa wingi kutoka kwa nusu ya county hizo 47.

Kwa mfano katika uchaguzi mkuu ujao, kuna miungano ya vyama vya kisiasa. Kuna ushirika baina ya chama cha ODM cha waziri Mkuu Raila Odinga ambaye anatoka kabila la Wajaluo na kile cha Wiper democratic cha makamu rais Kalonzo Musyoka ambaye anatoka kabila la Wakamba ambapo muungano huo pia umejumuisha vyama vidogo vidogo 11 na kuunda muungano wa Cord. Mmoja wa viongozi hawa anatokea eneo la magharibi mwa Kenya ilihali mwingine anatokea eneo la mashariki mwa Kenya.

Pia ushirika wa kisiasa baina ya Uhuru Kenyatta ambaye anatoka kabila la Wakikuyu na William Ruto anayetoka kabila la Wakalenjin umetokana na sababu hizo hizo za kujaribu kupata wingi wa kura. Bwana Kenyatta anatokea chama cha TNA, na ameunganisha nguvu na vyama vya URP, UDFna Rainbow Coalition ili kuunda muungano wa Jubilee.

Bwana Kenyatta anatokea eneo la Kati la Kenya ilihali bwana Ruto anatokea mkoa wa Rift Valley. Wagombea wengine wote wa kiti cha urais pia wameunda ushirika na viongozi wa vyama kutoka makabila mengine. Lengo lao likiwa hilo, hilo la kupata ushindi.

Wanasiasa wengine ambao wanawania urais ni pamoja na Peter Keneth mbunge wa jimbo la gatanga ambaye anawania nafasi ya juu ya uongozi kwa tiketi ya muungano wa Eagle ambao umetokana na vyama vya KNC na POA. Mgombea mwenza ni Ronnie Osumba, naye mwanasiasa mkongwe Musalia Mudavadi anawania urais kupitia muungano wa amani ambao umeunganisha vyama vya UDF, New Ford Kenya na KANU na mgombea mwenza wake ni Jeremiah Kioni.

Mwanamke pekee katika kuwania nafasi ya urais ni mwanasiasa machachari Martha Karua kwa tiketi ya NARC kenya na mgombea mwenza wake ni Augustine Lotodo. Na mwanamke pekee aliyeteuliwa kuwa mgombea mwenza katika uchaguzi huu ni Winnie Kinyua kwa tiketi ya Restore and Build kenya ambapo mgombea urais ni Prof. James Kiyiapi.

Mwanasiasa mashuhuri Paul Muite yeye anawania nafasi ya urais kupitia chama chake cha Safina na mgombea mwenza wake ni Shem Odhuodho, wakati mgombea urais Mohammed Abduba Dida ambaye hajulikani katika siasa za Kenya anaingia uwanjani kwa tiketi ya Alliance for Real Change na mgombea mwenza wake ni Joshua Onono.
XS
SM
MD
LG