Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Aprili 19, 2024 Local time: 23:56

UN Uturuki na Somalia kufanya mkutano wa kimataifa


Umoja wa Mataifa, Uturuki na Somalia zitaandaa kwa pamoja mkutano wa kimataifa juu ya Somalia wiki ijayo huko Istanbul.

Umoja wa Mataifa, Uturuki na Somalia zitaandaa kwa pamoja mkutano wa kimataifa juu ya Somalia wiki ijayo huko Istanbul. Mkutano huo wa maafisa wa vyeo vya juu utazingatia masuala ya usalama wa Somalia, ushirikiano wa kisiasa na kazi za kuikarabati nchi pamoja na namna ya kukabiliana na uharamia.

Mkutano huu wa siku tatu utaanza Ijumaa ijayo na kuhudhuriwa na katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon pamoja na marais kadhaa na mawaziri wakuu wa kigeni.

Balozi wa Uturuki kwenye Umoja wa Mataifa, Ertugrul Apakan, aliwaambia wajumbe wenzake wa baraza la usalama Alhamisi kuwa mkutano huo unatarajia kuonyesha nia ya jumuiya ya kimataifa kuhusiana na utaratibu wa amani wa Djibouti. Alisisitiza kuwa hautakua mkutano wa kuchangisha fedha, lakini utatoa nafasi kwa wawekezaji wa biashara wa kimataifa kujadili uwezekano wa biashara katika siku zijazo.

β€œPia mkutano utazingatia juu ya kazi za kufufua na kukarabati nchi kwa kuvutia uwekezaji wa moja kwa moja katika miradi ya miundo mbinu ambayo itaimarisha uchumi wa Somali, na kubuni ajira na kuleta mapato. Hii pia itaimarisha biashara za ndani ya nchi na kupelekea kuwepo maendeleo ya kijamii na kiuchumi na kuchangia kwa utaratibu wa amani.”

Wataalam wa vyeo vya juu wa Somalia wanasema kuimarisha maendeleo ya kiuchumi na kubuni ajira ni muhimu ili kuwazuiya vijana wa kisomali kuungana na makundi yenye siasa kali na kushiriki katika vitendo vya uharamia jambo ambalo limeota mizizi kwenye pwani ya Somalia.

Mkutano huu wa Istanbul unafanyika mwaka mmoja baada ya mkutano wa wafadhili wa Somalia huko Brussels. Zaidi ya dola millioni mia 2 ziliahidiwa kuisaidia serikali ya mpito na kikosi cha wanajeshi elfu 7 wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika-AMISOM. Umoja wa Mataifa unasema takriban dola millioni 150 ya fedha hizo tayari zimeshapokelewa.

Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Somalia, Ahmedou ould Abdallah, alisema mkutano wa Istanbul utawaonyesha wasomali na viongozi wao kwamba kuna jitihada kubwa inayofanywa na jumuiya ya kimataifa kutaka kufanya kazi nao.

Katika ripoti yake ya hivi karibuni juu ya hali huko Somalia ambayo ilitolewa wiki hii, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon, anasema licha ya changamoto nyingi serikali ya mpito imekuwa ikifanya juhudi kubwa za kuimarisha usalama na uthabiti nchini Somalia, lakini alionya kuwa alikuwa na wasiwasi kuwa serikali yao bado inategemea sana fedha za msaada wa kigeni.

​
XS
SM
MD
LG