Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Aprili 24, 2024 Local time: 12:40

UN yaitaka DRC kuheshimu haki za binadamu


Wafuasi wa upinzani na polisi wa kupambana na ghasia nje ya ofisi moja ya posta mjini Kinshasa, Octoba 13, 2011
Wafuasi wa upinzani na polisi wa kupambana na ghasia nje ya ofisi moja ya posta mjini Kinshasa, Octoba 13, 2011

Ripoti ya Umoja wa Mataifa imeitaka serikali ya Congo kuhamasisha na kuheshimu haki za binadamu wakati nchi hiyo ikielekea katika uchaguzi mkuu

Umoja wa Mataifa inasema ukandamizaji wa haki za msingi unaoendelea kufanywa kuelekea uchaguzi ujao wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo-DRC unahatarisha utaratibu wa kidemokrasia na unaweza kupelekea ghasia baada ya uchaguzi.

Ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa ilitoa ripoti Jumatano ikielezea takriban kesi 200 za ukiukaji wa haki za binadamu unaohusishwa na utaratibu wa uchaguzi, kati ya mwezi Novemba mwaka 2010 na Septemba mwaka 2011.

Inasema ukiukaji mwingi uliwahusisha polisi wa taifa la Congo-PNC au idara ya upelelezi ya taifa kuwalenga wanachama au wafuasi wa vyama vya upinzani. Pia kulikuwa na ghasia zilizofanywa na wafuasi wa vyama vya siasa.

Ripoti inasema raia walitishwa, kupigwa na kukamatwa mara kadhaa na maafisa wa PNC, kwa sababu tu ya kuvaa fulana za vyama vya upinzani.

Katika kesi moja, wanachama wawili maarufu wa taasisi ya taifa ya haki za binadamu walipewa vitisho vya kuuwawa baada ya kufanya mkutano na waandishi wa habari na kupinga marekebisho ya katiba.

Umoja wa Mataifa inaisihi serikali na viongozi wa kisiasa kuhamasisha na kuheshimu haki za binadamu. Pia inaitaka jumuiya ya kimataifa kuongeza juhudi zake katika kutoa mafunzo kwa majeshi ya usalama ya DRC, ambapo inasema wanalipwa mishahara midogo na hawana mafunzo bora na vifaa.

Kampeni tayari zimeanza kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa Novemba 28, ambapo Rais Joseph Kabila anakabiliwa na upinzani uliogawanyika.

Mmoja wa wapinzani wake wakuu ni Etienne Tshisekedi, mwenye umri wa miaka 78 mwanasiasa mkongwe ambaye alisusia kinyang’anyiro cha urais cha mwaka 2006.

XS
SM
MD
LG