“Leo ni hatua muhimu na madhubuti,” Guterres amewambia waandishi wa habari kuhusu maendeleo katika mazungumzo ya Istanbul kati ya pande nne.
“Hatua kuelekea kufikia makubaliano ya kina.”
Guterres amevunja ukimya kuhusu mazungumzo hayo, akigusia taarifa ya waziri wa ulinzi wa Uturuki, ambaye amesema kuna makubaliano kuhusu masuala muhimu, ikiwemo kuunda kituo cha uratibu na Russia, Ukraine na Umoja wa mataifa, makubaliano ya kukagua nafaka bandarini, na kuhakikisha usalama wa meli zinazosafirisha nafaka hizo nje ya bandari ya Odesa.
Wakati Guterres hakuweza kutabiri lini makubaliano ya mwisho yatakuwa tayari, amesema anatumai pande zote zitakutana tena wiki ijayo na kufikia makubaliano ya mwisho.
Zaidi ya tani milioni 20 za nafaka za Ukraine zinahifadhiwa kwenye ghala kwenye bandari ya bahari nyeusi ya Odesa, na darzeni ya meli zimekwama kwa sababu ya kikwazo cha Russia.
Uturuki ilisema ina meli 20 za kibiashara zinazosubiri katika eneo hilo ambazo zinaweza kupakiwa kwa haraka na kupelekwa kwenye masoko ya dunia.