Ujumbe wa wafanyabiashara wa India wenye wanachama 50 unaanza ziara ya siku nne nchini Russia Jumatatu wakati nchi zote mbili zikitaka kuimarisha uhusiano wa kiuchumi ambao umekua baada ya Russia kuivamia Ukraine.
India na Russia pia ziko katika mazungumzo ya makubaliano ya biashara huru, mawaziri kutoka nchi hizo mbili walisema mapema wiki hii wakati wa ziara ya Naibu Waziri Mkuu wa Russia, Denis Manturov mjini New Delhi. Katika miezi ya hivi karibuni, Moscow imekuwa muuzaji mkubwa wa mafuta ghafi kwa India huku Russia ikipigwa na vikwazo na hivyo kutafuta biashara zaidi na nchi za Asia.
New Delhi haijajiunga na vikwazo vya Magharibi vinavyoongozwa na Marekani dhidi ya Moscow au kulaani moja kwa moja uvamizi wa Russia kwa Ukraine lakini imekuwa ikitoa wito wa suluhisho la mashauriano kwa mzozo huo.