Waasi wa Sudan Kusini wanasema majenerali wao wakuu 23 wanatarajiwa kuwasili mjini Juba Jumatatu ijayo kujiandaa kwa ujio wa kiongozi wao, Riek Machar, ambaye alichaguliwa kuwa makamu rais wa kwanza katika utaratibu wa kuunda serikali ya umoja wa kitaifa.
Machar ameripotiwa kusema kwamba atasafiri kwenda Juba iwapo tu takriban wanajeshi wale 3,000 na polisi watakubaliwa kubaki katika mji mkuu na polisi wengine 1,200 wanawekwa kwenye miji ya Bor, Malakal na Bentiu.
Wakati huo huo utekelezaji wa mkataba wa amani wa Agosti 2015 umekuwa wa taratibu huko wote waasi na serikali ya Rais Salva Kiir wakitofautiana juu ya masuala kama uamuzi wa Rais Salva Kiir wa kuunda majimbo mapya 28, pamoja na kulaumiana kuhsu ukiukaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano.