Timu za Ureno, Uhispania, na Iran zitasubiri michezo yake ya mwisho kujua hatma zao za kusonga raundi ya pili huku Morocco ikiaga michuano ya Kombe la Dunia Russia 2018.
Kutokana na idadi ya pointi katika kundi B, timu yoyote inaweza kuifuata Morocco kurejea nyumbani. Uhispania inaongoza kundi hilo ikiwa na pointi 4, Ureno pointi 4 na Iran ikiwa na pointi 3.
Japokuwa timu ya Iran ilipoteza mchezo wake wa pili dhidi ya Uhispania Jumatano, ushindi dhidi ya Ureno katika mchezo wake wa mwisho unaweza kuifanya timu hiyo kuwa na pointi 6 na kufuzu.
Mpaka sasa timu zilizo ingia raundi ya pili ni wenyeji Russia na Uruguay kuktoka kundi A, huku Saudi Arabia na Misri zikishindwa kuvuka raundi ya pili ya mtoano.
Magoli ya Christiano Ronaldo kwa Ureno, na Diego Costa kwa Uhispania yalizipa nafasi nzuri timu hizo ya kusonga mbele baada ya mchezo wa kwanza kutoka suluhu (3-3).
Alhamisi itashuhudia michezo ya kundi C na D ambapo mpaka mwisho wa siku mwelekeo wa kundi C utafahamika. Denmark itacheza na Australia, Ufaransa na Peru na Argentina itapambana na Croatia.