Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Aprili 26, 2024 Local time: 22:39

Uganda yarudi nyuma katika vita dhidi ya Ukimwi


Daktari anachukua damu kupima ikiwa kuna virusi vya HIV huko Lagos Nigeria
Daktari anachukua damu kupima ikiwa kuna virusi vya HIV huko Lagos Nigeria
Miaka ya tisini Uganda ilipiga hatua kubwa sana kwenye vita dhidi ya ukimwi lakini sasa mambo yamebadilika. Kwa mujibu wa takwimu za tume ya ukimwi nchini Uganda, watu mia nne wanaambukizwa Ukimwi kila siku nchini Uganda. Takwimu hizi zimeifanya Uganda kuwa nchi ya kipekee mashariki na katikati mwa Afrika ambako kesi za uambukizwaji wa ukimwi zinaongezeka.

Wengi walio na virusi vya ukimwi wakiwa na umri wa kati ya miaka 15-40.

Huku Uganda ikiadhimisha siku ya kimataifa ya Ukimwi, wanaharakati wa kupambana na ukimwi wameamua kauli mbiu ya mwaka huu iwe "Kuzishirikisha upya jamii ili ziweze kuzuia uambukizaji wa ukimwi kikamilifu".
please wait

No media source currently available

0:00 0:06:23 0:00
Kiungo cha moja kwa moja

Wakati wa miaka ya tisini wakati Uganda iliweza kupambana na ukimwi, serikali ilisisitiza njia tatu za kinga. Kwanza, kutoshiriki ngono, pili, kuwa mwaminifu kwa mpenzi wako na tatu kutumia mipira ya condom maji yanapozidi unga, mashuhuri ikijulikana kama ABC

Sasa Uganda imelegea na ugonjwa huu umeanza kuwa kitisho tena kwa afya ya waganda. Ni kwa nini hili linafanyika? Mkurugenzi wa tume ya ukimwi nchini Uganda daktari David Apuuli anasema,.

"Tulikosea kwa sababu tuliwacha kuangazia sana tabia na maadili na kutilia mkazo njia za kisayansi za kupambana na ukimwi. Tulitilia mkazo madawa yanayopunguza makali ya ugonjwa huu pamoja na mipira ya condom. Hapo awali rais alikuwa amewaagiza wanasiasa wote kuwa kabla ya kumaliza hotuba zao, ni lazima wazungumzie suala la ukimwi. Hata kanisani baada ya kuubiri, makasisi walizungumzia ukimwi".

Tume ya ukimwi inasema kosa lingine lilitokea wakati mashirika mbali mbali yalipoanza kusambaza ujumbe ambao haukueleweka vizuri na watu. Kwa mfano utayaona matangazo yanayosema " Umeshiriki ngono na zaidi ya mtu mmoja? tumia condom, mpenzi wako kalala na mtu mwingine? Nenda ukapimwe."

Sasa, daktari Apuuli anasema kabla ya ujumbe wote wa ukimwi kutangazwa, itakuwa ni lazima uithinishwe na tume ya ukimwi kama njia ya kuhakikisha kuwa wananchi wanapata ujumbe unaofaa.

Mkurugenzi mkuu wa shirika la umoja wa mataifa la UNAIDS nchini Uganda bwana Musa Bungudu alisema mipango ya kupanbana na ukimwi haifai kutegemea sana ufathili kutoka nchi za kigeni kama itadumishwa. Pendekezo lake?

"Sisi sote tulio hapa tuna simu. Itakuwa bora kama tutatozwa kiasi kidogo cha pesa wakati tunapopiga simu ili pesa hizi ziende kwenye mfuko wa kupambana na ukimwi. Hili pia linafaa kufanyika kwa kila chupa ya pombe unayonunua. Tukifanya hivyo najua tunaweza kupata dola milioni mia tatu kila mwaka za kusaidia miradi ya ukimwi".

Uganda sasa inatilia mkazo zoezi la kuhakikisha kuwa hakuna mtoto anayezaliwa akiwa na virusi vya ukimwi.

Tume ya ukimwi inasema kesi nyingi za maambukizi ni miongoni mwa watu wanoishi na wapenzi wao au watu ambao wameoana na hii ndio sababu wanatilia mkazo njia za kuhakikisha kuwa wamama wajawazito hawawambukizi watoto wao virusi wakati wanapojifungua.

Hii ndio sababu watafiti kutoka Uganda wakishirikiana na Chuo kikuu cha Washington Marekani na watafiti kutoka nchi mbali mbali duniani kote mwaka uliopita, wakafanya

Utafiti wa kutafuta njia za kuhakikisha kuwa mtu aliye na virusi vya ukimwi na ambaye ana uhusiano wa mapenzi na mtu asiye na virusi hivi hatomwambukiza mwenziwe virusi hata wakishiriki ngono bila kinga.

Daktari Jonathan Wangisi mkuu wa utafiti kwenye shirika la kuwasaidia watu wanaoishi na virusi vya ukimwi la TASO nchini Uganda ni mmoja wa watafiti walioshiriki kwenye utafiti huu. Anatueleza hatua ya pili waliyochukua.

"Tulikuwa na dawa ya kupunguza makali ya ukimwi maarufu kama ARV ambayo tuliwapa watu ambao hawakuwa na virusi vya ukimwi lakini wakiwa na ushirikiano wa kimapenzi na watu wanaishi na virusi vya ukimwi na tulidhani hilo litamsaidia mtu asiye na virusi hivi asivipate".

Ujuzi wanaotumia Daktari Wangisi anasema ni sawa na ule unaotumiwa na watu kutoka mabara mengine wakija barani Afrika. Wao hunywa madawa fulani ya kujikinga wasiugue ugonjwa wa malaria.

Washiriki kwenye utafiti huu walikaguliwa kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita na dawa waliyopewa inaitwa tenofovir na truvada na matokeo yake anasema ."yalithibitishwa kuwa Tenofovir ilizuia maambukizi kwa asili mia 67 nayo truvada ikazuia maambukizi kwa asili mia 70".

Ukizingatia asili mia hii ya kupunguza maambukizi, daktari Wangisi anasema ikiwa mtu unayeshiriki ngono naye anakunywa dawa za kupunguza makali ya ukimwi, hii inamaanisha kuwa idadi ya virusi vya ukimwi vilivyo kwenye damu yake vinapungua kwa hivyo akishiriki ngono na mtu ambaye naye amekunya dawa za aina ya Truvada na tenofovir, basi uwezekano wa kuambukizwa unapungua sana sana na motto anayezaliwa hatakuwa na virusi vya ukimwi.

Hata hivyo, Daktari Wangisi anaonya kuwa dawa hizi zinafaa kutumiwa wakati wapenzi wanataka kujifungua au masaa 72 baada ya mtu kubakwa na anahofia huenda ameambukizwa virusi vya ukimwi.

Takwimu za tume ya ukimwi nchini Uganda zaonyesha kuwa idadi ya watoto wanaoambukizwa ukimwi imepungua. Mwaka wa elfu mbili kumi na moja, watoto elfu 25 walizaliwa wakiwa na virusi, mwaka wa elfu mbili na kumi na mbili kesi zikapungua hadi elfu 15 na mwaka huu kufikia mwezi wa kumi kesi hizi zilikuwa zimepungua zaidi na kufikia elfu nane.

Huku utafiti wa kupata tiba ya ugonjwa wa ukimwi ukiwa ungali unaendelea duniani kote, wataalam wa ugonjwa huu wanasema ikikumbukwa kuwa asili mia 99 za kesi za maambukizi ni kupitia ngono, njia dhabiti ya kupambana na ukimwi ni kuwa mwaminifu kwa mpenzi mmoja au kutoshiriki ngono ikiwa hujafunga ndoa.
XS
SM
MD
LG