Kiongozi mmoja wa upinzani nchini Uganda ameiomba mahakama ya kimataifa ya uhalifu-ICC- kumchunguza Rais Yoweri Museveni kwa shutuma za uhalifu wa kivita.
Olara Otunnu anasema alitoa ombi hilo Alhamisi wakati wa mkutano na Mwendesha Mashtaka Mkuu wa ICC, Luis Moreno-Ocampo, ambaye yupo nchini humo akihudhuria mkutano wa ICC.
Otunnu aliwaambia waandishi wa habari aliwasilisha ushahidi kuhusiana na shutuma za mauaji ya halaiki huko kaskazini mwa Uganda, uhalifu wa vita uliofanywa na majeshi ya Uganda nchini DRC, na vifo vya watu 30 wakati wa mapigano katika mji mkuu wa Uganda mwaka jana.
Hakukuwa na majibu ya haraka kutoka kwa Rais au wasaidizi wake. Moreno-Ocampo aliwaambia waandishi wa habari ataipitia taarifa hiyo. ICC imechunguza vita vya muda mrefu kati ya serikali ya Uganda na kundi la uasi la Lord’s Resistance Army-LRA.
Mwaka 2004 mahakama iliwafungulia mashitaka viongozi watano wa LRA kwa shutuma za uhalifu dhidi ya raia, lakini haijawafikisha mahakamani maafisa wowote wa Uganda.