Maafisa wa usalama nchini Uganda wametegua kifaa kinachoaminika kuwa ni bomu, kilichokuwa kimetegwa kwenye kituo cha mabasi kaskazini mwa nchi hiyo kwenye mji wa Gulu karibu na mpaka na Sudan kusini.
Raia waligundua kifaa hicho Jumatatu mchana na kuwaita polisi pamoja na wanajeshi walikitegua kwa haraka bila kukikagua wakisema kwamba kilikuwa karibu kulipuka.
Wapelelezi nchini humo wanaendelea na uchunguzi wao wakisema kwamba mabaki ya vifaa yamepelekwa maabara kwa uchunguzi zaidi na kuwatafuta wahusika waliotega kifaa hicho kinachoaminika kama kingelipuka kingeweza kujeruhi au kuuwa watu walio mita hamsini za mraba kutoka pale kilipokuwa.
Mji wa Gulu unaopakana na Sudan Kusini ulishuhudia umwagikaji mkubwa wa damu wakati wa vita vilivyoongozwa na kundi la waasi la Lord’s Resisitance Army linaloongozwa na Joseph Kony.