Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumapili, Julai 14, 2024 Local time: 13:05

Uchaguzi wa Kenya huwa na ushindani mkali, ghasia


Afisa wa polisi wa Kenya akiwa amembeba mwanafunzi na kumepeleka sehemu salama baada ya kutokea makabiliano kati ya polisi na waandamanaji katika mtaa wa Kawangware, jijini Nairobi. Oct. 30, 2017. Hii ni baada ya kutangazwa matokeo ya uchaguzi yaliokumbwa na utata.
Afisa wa polisi wa Kenya akiwa amembeba mwanafunzi na kumepeleka sehemu salama baada ya kutokea makabiliano kati ya polisi na waandamanaji katika mtaa wa Kawangware, jijini Nairobi. Oct. 30, 2017. Hii ni baada ya kutangazwa matokeo ya uchaguzi yaliokumbwa na utata.

Wadau mbali mbali wana imani kwamba uchaguzi wa mwaka huu nchini Kenya utakuwa wa amani tofauti na miaka ya nyuma, ni wakati Wakenya watajielekeza Agosti 9 kwenye vituo vya kupigia kura kumchagua rais mpya, wabunge, maseneta na wawakilishi wa kaunti .

Taifa hili la Afrika mashariki lina historia mbaya ya kugubikwa na machafuko yanayochochewa na ghasia za kikabila.

Mara nyingi ghasia hizo hutokea kwa sababu mmoja wa wagombea anakuwa amepinga matokeo ya uchaguzi au kwa sababu ya uhasama wa kikabila ambao inaelezewa mara nyingine huchochewa na wanasiasa.

Mifano ya chaguzi zilizogubikwa na ghasia

Uchaguzi wa vyama vingi wa mwaka wa 1997 uligubikwa na ghasia zilizopangwa dhidi ya makundi kutoka eneo la Rift Valley na mikoa ya pwani ambao walikuwa wanachukuliwa kama wapinzani wa chama tawala cha KANU.

Wakati huo, watu 100,000 walihamishwa kwenye makazi yao na wengine 400 kuuawa.

Uchaguzi wa 2007 ndio uligubikwa na ghasia mbaya ambapo zaidi ya watu 1,100 waliuawa na wengine 630,000 kuhamishwa kwenye makazi yao, wengi wao wakitoka Rift Valley.

Ghasia za kabla na baada ya uchaguzi huo, ilikuwa pamoja na jeshi la polisi kutumia nguvu za kupita kiasi na kuwafanyia vitisho raia, wanawake kubakwa na maafisa wa polisi, matumzi ya risasi za moto dhidi ya waandamanaji, mashambulizi ya vijana wenye silaha kama vile Mungiki dhidi ya wafuasi wa muungano wa vyama vya upinzani (ODM), na mashambulizi ya makundi yanayoshirikiana na ODM kama vile jeshi la ulinzi wa ardhi la Sabaot dhidi ya wafuasi wa chama cha Rais Kibaki cha National Unity.

Machafuko hayo yalipelekea Uhuru Kenyatta na William Ruto kufunguliwa mashtaka ya uhalifu dhidi ya ubinadamu na mahakama ya kimataifa ya uhalifu ya mjini the Hague (ICC) mwaka wa 2012.

Lakini mwaka wa 2014, waendesha mashtaka wa ICC waliondoa mashtaka dhidi ya Kenyatta kwa madai kwamba mashahidi walifanyiwa vitisho ili kubadili ushuhuda wao.

Miaka miwili baadaye, ICC ilitupilia mbali kesi dhidi ya Ruto kwa sababu ya ukosefu wa ushahidi wa kutosha.

Hisia za wachambuzi na wadau wengine kuhusu uchaguzi wa mwaka huu

Mchambuzi wa siasa Dismas Mokua , anasema mmoja ya mambo yaliyokuwa yanasababisha vurugu katika uchaguzi wa miaka iliyopita, ni wakati rais aliye madarakani anawania muhula wa pili.

Lakini mwaka huu, rais anayeongoza hatakuwepo kwenye kinyang’anyiro.

“Rais anapomaliza muhula wa kwanza, halafu anatafuta kuwania muhula wa pili, mara nyingi hapo ndipo tunakuwa na siasa mbaya, tunakuwa na vurugu, watu wanapigana, hata vifo kutokea na mali kuharibiwa,” anasema Dismas.

Dismas anasema inaonekana pia mwaka huu, “serikali imeweka mikakati madhubuti kuhakikisha uchaguzi unafanyika bila vurugu.”

“Jambo lingine ambalo linatia moyo ni kwamba katika kampeni za mwaka huu, wagombea wakuu wananadi zaidi sera kuliko kuomba watu kutoka kabila lao wawapigie kura,” ameongeza

Upande wa tume ya kitaifa ya utangamano na uwiano (NCIC), nao pia wanasema kuna tofauti kubwa kati ya uchaguzi wa mwaka huu na uchaguzi wa miaka iliyopita.

“Wakati huu kuna utulivu kuliko mwaka wa 2017, kwa hiyo tunaona kwamba tunaelekea kuwa na uchaguzi ambao hautakuwa na vurugu,” anasema Samuel Kobia, mwenyekiti wa NCIC.

Kobia anasema wadau mbali mbali wameshirikiana kuhakikisha uchaguzi wa mwaka huu unakuwa huru na wazi, na unafanyika kwa amani na utulivu.

“Katika kazi yetu ya kuzuia matamshi ya chuki, tumeshirikiana na wadau wengine, kufikia sasa tumeona kwamba matamshi ya chuki yamepungua kuliko ilivyokuwa miezi kadhaa iliyopita. Jambo lingine, tume ya uchaguzi na mipaka (IEBC) imejianda vya kutosha, na Wakenya wengi wameanza kuwa na imani na IEBC,” ameongeza.

Mapema wiki hii, IEBC imeiambia VOA kwamba iko tayari kuandaa uchaguzi wa Agosti 9 kwa njia ya uwazi, inayoaminika na inayoweza kuthibitishwa na kuwataka wanainchi wa Kenya kuwa na imani nayo.

Ripot hii imeandaliwa na Patrick Nduwimana, VOA, Washington DC

XS
SM
MD
LG