Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Februari 23, 2024 Local time: 06:04

Uchaguzi Angola: Joao Lourenco anatafuta muhula wa 2, upinzani umetishia kutumia njia zote kupinga matokeo


Rais wa Angola Joao Lourenco (kulia) ambaye anagombea mhula wa pili madarakani kwa chama cha MPLA.
Rais wa Angola Joao Lourenco (kulia) ambaye anagombea mhula wa pili madarakani kwa chama cha MPLA.

Wapiga kura nchini Angola wanajiandaa kupiga kura Jumatano Agosti 24 2022 kumchagua rais mpya. Uchauzi huo umetajwa kuwa na ushindani mkali kuwahi kushuhudiwa tangu kuanza kwa siasa za vyama vingi mwaka 1992.

Chama cha Peoples Movement for the Liberation of Angola – MPLA, kimetawala Angola tangu tangu nchi hiyo kujipatia uhuru kutoka kwa Ureno mwaka 1975.

Chama kikuu cha upinzani cha The National Union for the Total Independence of Angola UNITA, kimepata umaarufu mkubwa sana nchini humo kinyume na ilivyokuwa katika uchaguzi wa awali.

Angola, ambayo ni mzalishaji mkubwa wa mafuta Afrika, ilikumbana na mapigano ya wenyewe kwa wenyewe yaliyodumu kwa muda wa miaka 27.

Tayari chama cha upinzani cha UNITA kimeishutumu serikali kwa kujaribu kulazimisha utawala wa chama kimoja, na kwamba kinafikiria kupinga matokeo ya uchaguzi, ambao chama hicho kinaona kwamba huenda usiendeshwe kwa njia ya haki.

Kiongozi wa chama hicho Adabberto Costa Junior, amesema kwamba utawala wa MPLA, hautaki kabisa Angola kuwa nchi yenye demokrasia.

Wasiwasi kuhusu uwazi katika uchaguzi

Baadhi ya wakosoaji wa serikali wameelezea wasiwasi kwamba huenda uchaguzi ukakosa kumpata mgombea aliyechaguliwa na wapiga kura, maana yake kwamba huenda ukajaa wizi wa kura.

Kuna waangalizi 2,000 pekee wanaofuatilia uchaguzi wa Angola, nchi ambayo ni kubwa mara mbili ya Ufaransa.

Hesabu ya mwisho ya kura itatangazwa mjini Luanda na baadhi ya vituo vya kupigia kuwa vimewekewa masharti ya kutotangaza matokeo hayo.

Chama kinachotawala cha MPLA, kimekataa maombi ya vyombo vya habari kujibu shutuma hizo na hakijatoa taarifa yoyote, lakini kilisema awali kwamba kitakubali matokeo ya uchaguzi huo.

‘Serikali imedhibithi taasisi za umma ikiwemo mahakama’

Wanasiasa wa upinzani na mashirika ya kiraia yameishutumu serikali ya MPLA kwa kudhibithi taasisi za serikali ikiwemo mahakama na vyombo vya habari.

Rais wa Angola Joao Lourenco, naye hajazungumzia shutuma hizo, lakini aliwahi kusema mwanzoni mwa mwaka huu kwamba mahakama za Angola zina uhuru wa kufanya kazi yake bila ya kuingiliwa.

Lourenco aliteuliwa na Jose Eduardo dos Santos, aliyeachia madaraka mwaka 2017, baada ya kutawala nchi hiyo kwa muda wa miaka 38.

Lourenco anagombea muhula wa pili, upinzani umetishia kupinga matokeo

Lourenco anagombea muhula wa pili madarakani.

Ameahidi kupambana na ufisadi, kuimarisha ukuaji wa uchumi na kuimarisha demokrasia.

Lakini Costa Junior amesema kwamba ahadi anazotoa rais wa sasa hazijawahi kutekelezwa na utawala wake, na kwamba hakuna mabadiliko yanayoonekana kutekelezwa ili kuimarisha hali ya maisha kwa watu wa Angola.

Costa amesema kwamba iwapo matokeo ya uchaguzi hayatakuwa huru na haki, watatumia njia zote za kitaifa na kimataifa, wanazoweza kuzitumia, kupinga matokeo hayo.

Amesema kwamba chama chake tayari kina ushahidi kwamba kanuni kadhaa za uchaguzi zimekiukwa lakini ana imani kwamba tume ya uchaguzi itatekeleza mabadiliko kuhakikisha uchaguzi unakuwa huru na wa haki.

Chama kinachotawala kimekataa kuzungumzia madai ya upinzani

Chama cha MPLA kimekataa kabisa kuzungumza na waandishi wa habari kuhusu madai ya upinzani.

Costa Junior amewataka wapiga kura kubakia kwenye vituo vya kupiga kura baada ya kupiga kura yao ili kuhakikisha kwamba hakuna udanganyifu unafanyika.

Ripoti ya taasisi ya usalama nchini Angola, imesema kwamba iwapo chama cha MPLA kinashinda uchaguzi wa leo, huenda kukatokea vurugu.

Mwili wa rais wa zamani Jose Eduardo dos Santos umewasili Luanda

Wakati wapiga kura wanatekeleza haki yao ya kikatiba, mwili wa aliyekuwa rais wa nchi hiyo Jose Eduardo dos Santos umerudishwa nchini humo.

Dos Santos alifariki akipatiwa matibabu nchini Spain, mjini Barcelona, mwezi Julai.

Mwili wa Eduardo dos Santos umewasili Luanda, baada ya kusubiriwa kwa muda mrefu.

Wachambuzi wamesema hatua ya mwili wa Santos kurudishwa nchini wakati wa uchaguzi ni ya kisiasa.

Mbona mwili wa Dos Santos umerudishwa wakati nchi ipo katika uchaguzi?

Mwili wa Santos umerudishwa Angola baada ya kutokea hali ya kutoelewana yakiwepo madai kwamba aliuawa.

Santos alifariki Julai 8 mwaka huu, akiwa na umri wa miaka 79 akitibiwa mjini Barecelona ambako alikuwa amelazwa kwa muda mrefu.

Kesi kuhusu kifo chake ilifikishwa mahakamani na binti yake Tchize dos Santos akidai kwamba huenda rais huyo wa zamani aliuawa. Baada ya uchunguzi wa kina kwa mwili wake, mahakama hata hivyo ilisema kwamba alikufa kifo cha kawaida baada ya kuugua.

Familia yake ilikuwa imetaka mwili wake kuzikwa Barcelona, lakini mahakama ikaamua kwamba urudishwe Angola.

Rais Lourenco, ametoa wito kwa wapiga kura kupigia kura chama kinachotawala, kama heshima kwa hayati Dos Santos.

Kulingana na wachambuzi, mazishi yake yatatumika kwa manufaa ya kisiasa.

Ufisadi wakati wa utawala wa Dos Santos, vikwazo vya Marekani

Japo aliteuliwa na Dos Santos, Lourenco aliagiza uchunguzi wa madai ya ufisadi wakati wa utawala wa Dos Santos uliohusisha mabilioni ya dola.

Marekani ilimuwekea vikwazo mwaka 2021, binti wa dos Santos kwa kuhusika katika kashfa ya mabilioni ya dola fedha za umma kwa manufaa yake binafsi. kashfa hiyo ilifichuliwa na waandishi wa habari wapelelezi mwaka 2020.

Wapiga kura wa Angola wanawachagua wabunge na rais.

Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC

XS
SM
MD
LG