Tume ya kupambana na ufisadi nchini Sierra Leone imesema kwamba inaweza kutoa hati ya kukamatwa kwa aliyekuwa rais wa nchi hiyo Ernest Bai Koroma, baada ya kukataa kufika mbele ya tume hiyo kwa mahojiano.
Mawakili wa Koroma wamesema kwamba Koroma alishindwa kufika mbele ya maafisa wa tume hiyo mjini Freetown, kutokana na hofu ya usalama wake.
Mkuu wa tume ya kupambana na ufisadi nchini Sierra Leone Francis Ben Kaifala, amewaambia waandishi wa habari kwamba tume hiyo inafikiria kutoa hati ya kutaka rais huyo wa zamani akamatwe.
Uchunguzi unaendelea dhidi ya uliokuwa utawala wa Koroma, kwa madai kwamba uliiweka nchi hiyo katika hali mbaya kiuchumi, karibu uanguke.
Uchunguzi huo unahusu sekta za madini, ujenzi na mikataba ya ununuzi iliyotolewa wakati wa utalwa wa Ernest Bai Koroma kati ya mwaka 2007 na 2018.
Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC