Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Novemba 02, 2024 Local time: 08:20

Rais Donald Trump atoa dira mpya kwa wafanyakazi


Rais Donald Trump akihutubia ulimwengu
Rais Donald Trump akihutubia ulimwengu

Bilionea maarufu katika biashara ya kumiliki majumba Trump ameapishwa Ijumaa na kuwa rais wa 45 wa Marekani.

Wakati wa wananchi kunufaika

“Huu ni wakati wenu wa kunufaika, “Trump aliwaambia zaidi ya watu laki tatu waliokusanyika katika viwanja vya Taifa, Washington kushuhudia kuapishwa kwake na kusikiliza hotuba yake ya kuingia madarakani, “Wananchi watakuwa tena watawala wa taifa hili.”

Wananchi waliohudhuria kushuhudia kuapishwa kwa Rais Donald katika eneo la kumbukumbu ya Lincoln ya taifa Washington
Wananchi waliohudhuria kushuhudia kuapishwa kwa Rais Donald katika eneo la kumbukumbu ya Lincoln ya taifa Washington

​Wakati mvua ilikuwa inanyesha kidogo kidogo, Trump mwenye umri wa miaka 70, ambaye sasa ndiye mtendaji wa ngazi ya juu wa Marekani mwenye umri mkubwa kuliko wote, amesema, “Dira mpya ndio itatuongoza kuanzia sasa kwenda mbele. Itakuwa ni Marekani kwanza. Naahidi sitowaangusha kabisa. Amerika itaanza kushinda, itashinda kuliko wakati mwengine wowote.

Maadamano dhidi ya Trump

Baada ya muda mfupi, wakati Trump anakirimiwa na viongozi wa bunge la Marekani kwa chakula cha mchana, maadamano ya kumpinga yaliibuka katika baadhi ya sehemu za Washington katika maeneo mbali kidogo kutoka kwenye njia ya gwaride la uzinduzi huo wa kuapishwa Trump. Mawe yalitupwa na waandamanaji walipambana na polisi, ambapo imeripotiwa kuwa zaidi ya 95 wamekamatwa.

Waandamanaji wanawake wakipinga sera za Rais Trump katika sherehe za kuapishwa kwake wanazuiliwa na polisi, Washington DC
Waandamanaji wanawake wakipinga sera za Rais Trump katika sherehe za kuapishwa kwake wanazuiliwa na polisi, Washington DC

Ikiwa amerejea yale yaliyokuwa katika kampeni yake ya kuingia ikulu ya White House, Trump wa chama cha Republikan alieleza hali ya wafanyakazi ambao wametelekezwa katika nchi yenye uchumi wa juu kuliko zote, walioyumbishwa na mabadiliko ya uchumi wa dunia na hawana uwezo wa kukabiliana nao.

Walikuwa ni hawa wapiga kura waliompa Trump ushindi katika majimbo makuu, wachambuzi wa siasa wanasema, kwa kuwa walimwezesha kupata ushindi aliokuwa hakuutarajia katika uchaguzi wa Novemba na kumshinda Hillary Clinton wa Demokratik, ambaye pia ni waziri wa mambo ya nje wa zamani aliyekuwa anamwangalia katika nafasi aliyokuwa amekaa katika sherehe hizo wakati ameshakuwa rais.

“Washington ilineemeka lakini watu hawakupata fursa ya kupata manufaa ya utajiri huo, “Trump alisema. “Wanasiasa waliendelea kunufaika lakini kazi ziliwakimbia wananchi na viwanda vilifungwa.”

“Hii balaa iliyoikumba Marekani lazima imalizike hapa na hivi sasa,” alitangaza.

Trump aliahidi kurejesha kazi zilizowapotea wamarekani kwa sababu ya biashara zilizohamia nje ya nchi, na kusema ataboresha ajira katika nyanja za kujenga tena miundo mbinu ikiwemo barabara, madaraja yaliyoanza kuharibika.

“Kwa hiyo kwa wamarekani wote, sikilizeni maneno haya,” alisema. “Hamuwezi kupuuzwa tena.”

Trump aligusia kidogo sana kuhusu sera ya mambo ya nje ya Marekani, akisema kuwa Marekani itafanya urafiki na ulimwengu wakati ikitambua kuwa nchi hizo zina haki ya kujitawala vile zinavyoona ni sawa.

Amesema Marekani itaendelea “kung’ara na kila mtu kuiiga.”

Aahidi kutokomeza ugaidi

Lakini alirejea ahadi yake aliyokuwa akiitoa mara nyingi kuangamiza “ugaidi wenye msimamo mkali wa kidini “akisema atauondosha kabisa na kuuangamiza uondoke duniani.”

Alikula kiapo cha heshima ambacho ni utamaduni wa kila rais aliyepita katika kuapishwa, nalo ni kuilinda na kuitetea katiba ya Marekani. Trump amemrithi ambaye sasa ni rais mstaafu Barack Obama, ambaye anaacha madaraka baada ya awamu mbili alizotumikia ikulu ya White House.

Kundi kubwa lilikuwa katika eneo la National Mall, lakini halikulingana na lile ambalo lilijitokeza mara ya kwanza 2009 Obama alipochukua madaraka.

Wengi kati ya wale walioshuhudia Trump akiapishwa kuingia madarakani walivaa kofia zenye chapa ya kauli mbiu ya Trump ya kampeni yake. “Ifanye Marekani iwe Bora Tena,” wakishangilia kwa sauti kubwa wakati alipomaliza kuapishwa kuwa rais.

Trump aapa

Rais Donald Trump akiapishwa
Rais Donald Trump akiapishwa

Trump alikula kiapo cha urais kwa kuapishwa na Jaji Mkuu John Roberts, akiweka mkono wake juu ya Bibilia mbili, moja aliyokuwa anaitumia toka utoto wake na nyingine iliyotumiwa tokea karne ya 19, na Abraham Lincoln, kiongozi wa Marekani aliyetawala wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Kabla ya hapo aliyekuwa Gavana wa Indiana, Mike Pence aliapishwa kuwa makamu rais mpya, akichukua nafasi ya Joe Biden.

Baada ya kutoa hotuba yake ya kuingia madarakani, viongozi wa bunge walimkirimu Trump, mkewe Melania, makamu rais Pence, mkewe Karen, na familia zao katika karamu ya chakula cha mchana kabla ya kuanza gwaride katika mataa wa Pennsylvania kuelekea White House, makazi mapya ya Trump.

XS
SM
MD
LG