Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Aprili 19, 2024 Local time: 22:24

Trump aendelea kupinga matokeo wakati Biden akijiandaa kukabidhiwa madaraka


Rais mteule Joe Biden (kushoto) na Rais Donald Trump.
Rais mteule Joe Biden (kushoto) na Rais Donald Trump.

Siku moja kabla ya wajumbe wa Electoral College kukutana ili kumpitisha rasmi Mdemokrat Joe Biden kuwa rais wa Marekani, Donald Trump anaendelea kupinga matokeo ya uchaguzi wa Novemba 3.

Maelfu ya wafuasi wake walikusanyika Washington Jumamosi wakiunga mkono juhudi za rais zilizofeli kubadilisha matokeo ya kushindwa kwake katika uchaguzi.

Mwanachama wa kikundi cha mrengo wa kulia Proud Boys akishikiliwa na polisi wakati wa maandamano ya kupinga matokeo ya uchaguzi mjini Washington, Marekani, Disemba 12, 2020
Mwanachama wa kikundi cha mrengo wa kulia Proud Boys akishikiliwa na polisi wakati wa maandamano ya kupinga matokeo ya uchaguzi mjini Washington, Marekani, Disemba 12, 2020

Uchaguzi wa urais Marekani haukamiliki mpaka wajumbe waliopewa mamlaka na katiba kutoka majimbo yote 50, waliochaguliwa kulingana na idadi ya wakazi na kuwakilisha majimbo yao katika Bunge, watakutana kupiga kura zao. Isipokuwa katika majimbo mawili tu ya Marekani, kila mjumbe kutoka katika jimbo wote wanapiga kura kwa mgombea wa urais aliyeshinda katika jimbo lao.

Wakati majimbo yote yamekwisha idhinisha matokeo ya uchaguzi, Biden alishinda kwa kura za wajumbe 306 --- kura 36 zaidi kuliko zile anazohitaji kuwa rais --- ikilinganishwa na Trump aliyepata kura 232. Bila ya amri ya mahakama ya kuchelewesha mchakato huo, wajumbe wanatarajiwa kukamilisha zoezi la kupitisha ushindi wa Biden siku ya Jumatatu.

Mahakama za serikali kuu na za majimbo zimetupilia mbali darzeni za mashtaka yaliyofunguliwa na Trump na washirika wake wakitaka matokeo kubadilishwa au kubatilishwa katika majimbo yenye ushindani mkubwa ambayo Biden alishinda kwa viwango vinavyotofautiana.

Hivi karibuni, Ijumaa jioni Mahakama ya Juu ya Marekani ilikataa kusikiliza kesi iliyofunguliwa na jimbo la Texas ikitaka matokeo ya majimbo manne yafutwe, na hivyo kufunga njia yoyote kwa Trump kubadilisha matokeo ya uchaguzi kupitia Mahakama.

Hata hivyo Trump ameendelea kupambana na kuashiria kuwa hajakata tamaa.

“Ndio Tumeanza mapambano,” rais aliandika katika ujumbe wake wa Twitter Jumamosi. Saa moja kabla, aliandika, “Nimeshinda uchaguzi kwa kishindo”.

Trump alianza kutuma ujumbe wa Twitter wakati maelfu ya wafuasi wake wakereketwa wakikutana mjini Washington ili kuandamana na kupaza sauti kwa ajili ya rais aendelee kuongoza.

Maandamano kama hayo yametokea katika majimbo kadhaa ya Marekani ambapo timu ya mawakili ya Trump zimeshindwa kupinga ushindi wa Biden mahakamani.

Mapambano ya ghafla yalizuka kati ya wafuasi wa Trump na wapinzani wake. Watu wanne walipelekwa hospitali baada ya kujeruhiwa kwa kuchomwa visu na wengine 23 kukamatwa, kulingana na idara ya polisi ya manispaa ya Washington.

XS
SM
MD
LG