Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Oktoba 04, 2024 Local time: 18:27

Trump aelekeza macho kwenye uchaguzi wa New Hampshire, baada ya kushinda Iowa


Donald Trump akihutubia wafuasi wake mjini Des Moines Iowa, Jumatatu usiku.Reuters Januari 15, 2024
Donald Trump akihutubia wafuasi wake mjini Des Moines Iowa, Jumatatu usiku.Reuters Januari 15, 2024

Kufuatia Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump kuibuka mshindi  Jumatatu usiku kwenye uchaguzi wa mapema wa kuidhinisha mgombea urais wa Repablikan, kwa kujipatia asilimia 51 ya kura zilizopigwa, macho yote sasa yanaelekezwa kwenye jimbo la New Hampshire.

New Hampshire itafanya uchaguzi wa awali wa kumuidhinisha mgombea wa chama cha Repablikan, Jumanne wiki ijayo. Wapinzani wa Trump kwenye zoezi hilo la Iowa walikuwa wameshindwa kwa asilimia kubwa akiwemo Gavana wa Florida Ron DeSantis akiwa na asilimia 21.2 ya kura zilizopigwa, akifuatiwa na Gavana wa South Carolina Nikki Haley kwa asilimia 19.1, na kisha mwanabiashara Vivek Ramaswamy akiwa na asilimia 7.7.

Wawaniaji watatu wa chama hicho, Trump, Desantis na Nikki Haley, ndio watakaomenyana wiki kesho, baaada ya muwaniaji wa nne, Vivek Ramaswamy kujiondoa kufuatia uchaguzi wa Jumatatu. Wengine wote walipata chini ya asilimia 1 ya jumla ya kura zilizopigwa.

Ushindi huo unampa motisha Trump kwenye uchaguzi sawa na huo wiki ijayo kwenye jimbo la New Hampshire, ambako Haley amekuwa akipata umaarufu mkubwa, kwa matumaini kwamba ataweza kushinda na kuleta mwamko mpya kwenye kampeni za Repablikan.

Mara ya mwisho kwa Trump kushiriki kwenye uchaguzi wa Iowa ilikuwa 2016 alipokuwa akitafuta uteuzi wa rais, ambapo alishindwa na Seneta wa Texas Ted Cruz, wakati huo akijipatia asilimia 24.3 ya jumla ya kura zilizopigwa.

Forum

XS
SM
MD
LG