Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Machi 02, 2024 Local time: 02:10

Tishio la al-Shabaab kwa wakimbizi Somalia


Watoto wa Somalia wenye njaa
Watoto wa Somalia wenye njaa

Njaa Somalia: Vitisho vya kundi la kigaidi la al-Shabaab

Katika mfululizo wa makala yetu maalum juu ya njaa katika Pembe ya Afrika, tunatupia jicho historia ya kundi la kigaidi la al-Shabaab, ambalo kwa muda mrefu liliyumbisha usalama wa Somalia na hata kuvuruga juhudi za mashirika fadhili kupeleka misaada ya chakula nchini humo.

Tishio la al-Shabaab lilikumba Somalia baada ya muda mrefu wa kutokuwepo na serikali thabiti. Serikali ya mwisho iliyokuwa thabiti iliongozwa na rais Mohammed Siad Barre aliyetimuliwa madarakani mwaka wa 1991.

Na kwa miaka 21 sasa, Somalia haijawa na serikali yenye udhibiti wa maeneo yote ya nchi. Marais pamoja na mawaziri wakuu walioteuliwa katika serikali ya mpito wametekeleza kazi zao kwa hofu na vitisho.

Mara wanashambuliwa na hata kuuawa na makundi yaliayoanza kama makundi ya waasi na hatimaye kupata nguvu na hata misaada ya kifedha ya nje. Isitoshe, serikali ya mpito ya Somalia, pia imekuwa ikipata pigo kutoka kwa maharamia wanaoteka nyara meli na hata watu katika pwani ya nchi hiyo. Fedha za fidia wanazodai maharamia hao hutumika kwa njia zisizoeleweka na kuongeza tishio kwa utawala wa taifa hilo.

Lakini wakati huu, Somalia imekumbwa na uhaba mkubwa wa chakula hasa katika maeneo ya kusini ya Bakool na Shabelle ambayo yamedhibitiwa kwa miaka na kundi la kigaidi la al-Shabaab.

Ni mwanzo wa mwezi wa Agosti ambapo kundi hilo la kigaidi la al-shabaab limelegeza kamba na yaripotiwa limetimuliwa nchini Somalia na vikosi vya serikali vikisaidiwa na vile vya Umoja wa Afrika. Lakini ikiwa kundi hili ambalo limeyumbisha usalama wa Somalia limeweza kutokomea kabisa nchini humo au la, ukweli utabainika baada ya muda.

Lakini turejelee historia ya usumbufu wa al- Shabaab kwanza. Kundi hili linahusishwa na mtandao wa kigaidi wa al-Qaida ambaye kiongozi wake Osama Bin Laden aliuawa mwezi Mei mwaka huu wa 2011.

Nchini Somalia ambapo kundi la al- Shabaab liliongozwa na gaidi Abdallah Fazul, nalo lilipata pigo baada ya Fazul kuingia katika mtego wa panya na kuuawa pia. Wachambuzi wanasema kufuatia kifo chake, al-Shabaab ilikosa mwongozo na uthabiti.

Lakini kwa wasomalia, kundi la al Shabaab limewaathiri kwa namna wengi nje ya Somalia hawawezi kuelewa. Mbunge Hussein Bantu wa bunge la Somalia anasema kundi hilo limejaa raia wa kigeni, wengine kutoka Pakistan na Afghanistan, na kwamba raia wa Somalia wanachama wa kundi hilo ni wachache.

Baada ya ukame na baa kali na njaa kukumba Somalia, raia wa kila tabaka walidhurika wakiwemo wanachama wa kundi hilo la kigaidi. Mwanzo walipiga marufuku mashirika kadha ya kimataifa hasa ya Kimarekani kupeleka misaada yoyote nchini humo.

Idara nyingi pia za Umoja wa Mataifa zililazimika kufunga operesheni zao za kibinadamu nchini Somalia. Mbunge Bantu aliieleza Sauti ya Amerika juu ya madhara yaliyotokana na vitisho vya al-Shabaab, ambapo raia wengi wa Somalia hasa kusini mwa nchini walilazimika kutembea kwa siku kuingia nchini Kenya ambapo kuna kambi za wakimbizi ili kuokoa maisha yao.

Ripoti ya Umoja wa Mataifa iliielezea Somalia kuwa mojawapo ya nchi hatari zaidi duniani kwa wafanyikazi wa kutoa misaada ya kibinaadam. Wafanyakazi 14 wa shirika la chakula duniani WFP waliuawa hapo mwaka wa 2008 na kundi la al Shabaab.

Kwingineko familia za wanachama wa kundi hilo la Al-Shabaab walijiandikisha kupokea posho za chakula cha mgawo. Wakati mwingine makundi hayo yalilazimisha mashirika fadhili kununua vyakula vya msaada kutoka kwa wakulima wa Somalia. Lakini hali imekuwa tete, huku kukiwa na ukame, njaa na hata uhaba wa fedha.

Mbunge Bantu anasema jamii ya kimataifa ingeliingilia kati zamani kuiokoa Somalia na magaidi kama hao wasio na utu, kama ilivyofanya katika nchi zingine za dunia. Mnamo mwisho wa wiki ya kwanza ya Agosti, kundi hilo la al- Shabaab liliripotiwa kudhoofika na kutimuliwa Somalia na vikosi vya serikali vikisaidiwa na vile vya Umoja wa Afrika na kwa mara ya kwanza wakaazi wa Mogadishu walipata sababu ya kusherehekea

Kundi la kigaidi la al Shabaab ambalo wasomali wanasema limekusanya raia wa kigeni wakiwemo wamarekani wenye asili ya kisomali sasa laripotiwa kutokomea nchini humo. Haijabainika wazi kilichooondoa udhibiti wa al-Shabaab Somalia.

Kuna hisia mchanganyiko,wengine wakidhania labda ni kutokana na mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan kwa waumini wa dini ya kiislam, njaa na ukosefu wa fedha, lakini ikiwa huu ndiyo mwisho wake, ukweli utabainika baadaye.

XS
SM
MD
LG