Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Mei 23, 2024 Local time: 03:20

Juhudi za kuwanasua vijana kutoka katika mihadarati zafanikiwa Kenya


Washiriki katika juhudi za kuachana na mihadarati
Washiriki katika juhudi za kuachana na mihadarati

Utafiti kutoka shirika la kupambana na mihadarati nchini humo NACADA wanaonyesha kuwa pwani ya nchi hiyo ni sehemu iliyoathirika zaidi kuliko sehemu nyingine.

Baadhi ya wanaotumia mihadarati eneo la pwani wameanza kuacha dawa hizo na kujitokeza hadharani, wakisaidiwa na mashirika ya kijamii.

Shirika moja la Reach Out Center linajihusisha na kuwafikia watumiaji mihadarati nchini humo limefanikiwa kunasua idadi kubwa ya waraibu wa mihadarati na kuwapa mafunzo maalum, na sasa vijana hao wanasaidia shirika hilo kuwatambua waraibu wengine na kuwanasua.

Mzungumzaji katika kongomano la kuachana na mihadarati
Mzungumzaji katika kongomano la kuachana na mihadarati

Shirika la Reach Out Center lenye makao yake mjini Mombasa limefanikiwa kuwanasua takriban vijana 100 pwani ya Kenya, ambapo vijana 80 kati yao tayari wamepewa mafunzo ya nyanjani.

Kulingana na utafiti wa hivi karibuni kutoka shirika la Umoja wa mataifa UN kitengo kinachoshughulika dawa ni kwamba Kenya ina takriban waraibu wa mihadarati elfu 18.

Mwandishi wa Idhaa ya Kiswahili VOA Salma Mohamed amesema vijana hao ambao sasa wamekuwa mfano mwema katika jamii, wamepewa jina la “Mwalimu.”

“Mimi nimetumia mihadarati kwa zaidi ya miaka 20, wazazi wangu walijaribu kunishauri lakini wakati huo sikuwa na nia ya kuacha. Lakini nilifanya maamuzi kujitokeza na kutafuta msaada, na saa hii naendelea na matibabu vizuri.” Amesema kijana mmoja.

Baada ya kupewa mafunzo maalum vijana hawa huajiriwa na shirika hilo ambapo jukumu lao ni kwenda mitaani kuwatafuta na kuzungumza na waraibu wengine.

Mwingine ni Bi.Mary Awuor ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 40.

Mary anasema aliposhindwa kuendelea na masomo akiwa bado msichana alijiingiza katika biashara ya ukahaba mjini Mombasa ambapo baadae alijikuta akitumia mihadarati kama vile bangi na dawa zingine hatari.

Anakiri kwamba alifanikiwa kupata watoto 4 wakati huo, lakini 3 kati yao aliwaua kwa kuwatupa, na sasa anajuta kwani amesalia na mtoto mmoja pekee ambaye ana umri wa miaka 20.

Aidha Mary amebadilika na kuacha tabia hizo, na sasa ameajiriwa na shirika la Reach Out kama afisa wa nyanjani ambapo anajipatia kipato cha kila siku huku akizunguka kuwanasua waraibu wengine mitaani.

“Sio kazi rahisi kwenda kuwashiwishi watu kuacha mihadarati lakini tunafanya kwa sababu tumejitolea. Jambo zuri ni kwamba wengi wao nawafahamu, wengine tulisoma pamoja na pia wanajua kuwa nilikuwa nikitumia mihadarati kama wao lakini nikaacha.” Amesema Mary.

Mkurugenzi mkuu wa shirika hilo Taib Abdulrahman ameiambia VOA kwamba kuwepo kwa bandari Mombasa kumechangia pakubwa usafirishaji wa dawa hizo, na hivyo imekuwa changamoto kwao.

Hata hivyo amesema mihadarati ni tatizo la ulimwengu mzima sio tu Kenya pekee.

“Ukiangalia nchi zote zilizoko karibu na bahari duniani zimeathirika na dawa za kulevya, hasa sehemu kuliko na bandari kwa sababu husafirishwa kwa urahisi zaidi. Mfano mzuri ni nchi jirani zetu Zanzibar, Visiwa vya Shelisheli, Mauritius hali ndio kama hivi unavyoona hapa, lakini bado tunaendelea kupambana.” Amesema Abdulrahman.

Idadi ya waraibu wa mihadarati hupata magonjwa hatari kama vile virusi vya Ukwimi, huku utafiti wa ukionyesha kuwa asilimia 18.3 ya wakenya wana virusi hivyo.

Imetayarishwa na Salma Mohamed, Mombasa, Kenya

XS
SM
MD
LG