Tanzania ni mwenyeji wa mkutano uliojumuisha marais sita wa nchi za Afrika Mashariki na Kati. Mkutano huo wa siku mbili uliofanyika jijini Dar es Salaam ulijadili suala la uwekezaji na changamoto za uboreshaji wa miundo mbinu katika kukuza biashara na masoko katika nchi za ukanda wa kati.
Viongozi wa Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda, na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo-DRC ni miongoni mwa waliohudhuria mkutano huo.
Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania alielezea kwenye mkutano huo nia yake ya kuboresha miundo mbinu ya usafiri wa reli na barabara kwenye eneo la ukanda wa kati nchini mwake ili kuwasaidia wananchi wa ukanda huo sambamba na uingizaji na usafirishaji bidhaa kwa nchi zisizo na bandari.
Miongoni mwa hatua ambazo Tanzania imechukua ili kuboresha sekta ya miundo mbinu kwa ajili ya kukuza ukanda wa kati unaotegemewa kwa usafirishaji wa mizigo na mataifa ya Uganda, Burundi, Rwanda na Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo-DRC ni kuboresha reli ya kati baada ya kuifanya kuwa mojawapo ya vipaumbele sita vya mpango wa matokeo makubwa hivi sasa.