Vijana hao wa Canada hao waliingia kwenye kinyang'anyiro hicho wakihitaji ushindi mbele ya watu 3,728 kwenye Uwanja wa DY Patil .
Amanda Allen aliipatia Canada bao la kwanza kwa mkwaju wa penalti. Lakini Tanzania hawakurudi nyuma waliendelea na mashambulizi na hatimaye Veronica Mapunda aliisawazishia Serengeti Girls.
Huku wakiwa wanahitaji ushindi, Wacanada walibadilisha mbinu za mchezo na kufanya mashambulizi makali lakini vijana wa Tanzania walisimama imara kwa uthabiti Canada walikosa umaliziaji kwani kunako dakika za lala salama shuti kali la Jade Bordeleau liliishia mikononi mwa kipa wa Tanzania.
Ikijulikana kwa jina la Serengeti Girls, Tanzania inashiriki kwa mara ya kwanza katika hafla ya Kombe la Dunia la FIFA. Na ilishtua dunia Jumamosi kwa ushindi wa 2-1 dhidi ya Ufaransa baada ya kufungwa 4-0 na Japan katika mechi yake ya kwanza.
Canada ilifungua mchezo kwa sare ya 1-1 na Ufaransa kabla ya kulazwa 4-0 na Japan siku ya Jumamosi.
Japan ilifikisha pointi 9 iliifunga Ufaransa 2-0 na kumaliza kileleni mwa kundi hilo. Tanzania pointi nne ilimaliza katika nafasi ya pili huku Canada ikiishia na pointi mbili ikimaliza ya tatu mbele ya Ufaransa yenye pointi moja.
Ufaransa ilishinda michuano hiyo mwaka 2012 huku Japan ikinyanyua kombe hilo mwaka 2014.
Timu mbili za juu katika kila moja ya makundi manne zinatinga robo fainali Japan dhidi ya Uhispania, Colombia dhidi ya Tanzania, Marekani dhidi ya Nigeria, na Brazil dhidi ya Ujerumani.
Uhispania ndio mabingwa watetezi, baada ya kushinda mwaka 2018 wakati Canada ilishika nafasi ya nne. Mashindano ya 2020 yalifutwa kwa sababu ya janga la Corona.