Serikali ya Tanzania ilitoa tamko maalum la kuanza utekelezaji rasmi wa sheria ya makosa ya mtandao ya mwaka 2015 na sheria ya miamala ya kielektroniki ambayo imekuwa gumzo kubwa tokea kupitishwa sheria hizo huku wengi wakiiona kwamba itanyima uhuru wa kutoa na kupata habari
Tamko la kuanza utekelezaji rasmi wa sheria hizo mbili yaani ya makosa ya mtandao ya mwaka 2015 na sheria ya miamala ya kielektroniki ya mwaka 2015 lilitolewa na Wizara ya Mawasilaiano, Sayansi na Teknolojia kupitia waziri wake, Profesa Makame Mbarawa. Sheria hizo zinaanza kutumika rasmi kuanzia Jumanne yaani Septemba mosi mwaka huu.
Profesa Mbarawa alisema licha ya kuwepo mafanikio katika matumizi ya mitandao, changamoto zilizojitokeza zilifanya serikali kutunga sheria hizo mbili.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar Es Salaam, Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Profesa Makame Mbarawa alisema hakuna ukweli wowote kwamba sheria hizi mbili zimeletwa ili kudhibiti uhuru wa mawasiliano kwa watanzania hususan wakati huu kuelekea uchaguzi mkuu ujao na kwamba wamejipanga ili kuhakikisha utekelezaji wake unakwenda kwa haki.
Kuanza kwa utekelezaji wa sheria hizi mbili za makosa ya mtandao ya mwaka 2015 na sheria ya miamala ya kielektroniki ya mwaka 2015 kunatokana na bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitisha hatua hiyo hapo April mosi mwaka huu.