Watanzania wameadhimisha miaka 62 ya uhuru wa Tanganyika wakiwa na maoni mbalimbali kuhusiana na maendeleo ya taifa hilo wakisema bado changamoto ni nyingi kwa wananchi ikilinganishwa na maendeleo yanayozungumziwa na viongozi.
Huku Rais Samia Suluhu Hassan akizindua mpango wa ushirikishwaji wananchi katika maandalizi ya Dira ya maendeleo ya Mwaka 2025-2050 suala ambalo limewaibua wanasiasa wakisema mpango huo wa ushirikishwaji wa wananchi umekuja kwa kuchelewa.
Wananchi hao wamesema wakati taifa hilo likiadhimisha miaka 62 ya uhuru bado maendeleo yamekuwa yanaonekana kwenye baadhi ya maeneo huku changamoto zikiwa ni nyingi ukilinganisha na maendeleo yaliyopatikana.
Anikazi Kumbemba mkazi wa Shinyanga anasema bado hali ya mwananchi mmoja mmoja kiuchumi haijaimarika kwa kuwa asilimia kubwa ya wananchi hao bado wanaishi kwenye umaskini.
“Bado hatujawasaidia Watanzania kwasababu hata hali zao kimaisha bado ni changamoto lakini maendeleo ya miundombinu tumejitahidi kwa kiasi chake lakini kwenye maendeleo ya mtu mmoja mmoja bado tuna changamoto kubwa sana miaka hii 62 ya uhuru wa Tanganyika” amesema Kumbemba.
Katika hotuba yake ya maadhimisho ya miaka 62 ya uhuru huko jijini Dodoma Rais Samia amezindua mchakato wa ukusanyaji maoni kuhusu Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 utakaowawezesha wananchi kutoa maoni yao juu ya Dira hiyo.
Suala ambalo wanasiasa wanaona limekuja kwa kuchelewa kwa kuwa Dira hiyo kwa asilimia kubwa imekwisha kuandikwa hivyo kushirikishwa kwa wananchi kwenye hatua hizo za mwisho ni kuwalaghai kama anavyoeleza Dkt Wilbroad Peter Slaa
“Mimi naona siyo kwamba wananchi wamechelewa kushirikishwa, hawajashirikishwa kinchofanyika hivi sasa ni namna ya kuwapamba tu wananchi kwamba watashirikishwa kwasababu huwezi kumshirikisha mtu ikiwa umekwisha andika asilimia kubwa ya Dira hiyo, utakuwa unakwenda kumshirikisha nini huyo mwananchi?”
Dira ya Taifa ni muhimu kwa mataifa yote duniani kwa kuwa ni mwongozo wa muda mrefu unaoweka malengo na matarajio ya maendeleo ya nchi kwa miaka mingi ijayo inajumuisha maono na malengo ya kijamii, kiuchumi, na kisiasa ambayo taifa linataka kufikia.
Dkt Vicent Stansilaus ambaye ni Mchumi na Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu huria Tanzania anasema ni muhimu kwa taifa la Tanzania kukipa kipaumbele kilimo katika Dira ya maendeleo ya mwaka 2050 kwa kuwa kilimo ndio uti wa mgongo wa taifa hilo.
Stanslaus anasema “Kama taifa tunategemea sana kilimo kiwe ndio uti wa mgongo wa uchumi wa nchi yetu kwasababu utakuta idadi kubwa ya Watanzania wanategemea kilimo kwahiyo ningetamani nguvu kubwa ielekezwe kwenye kilimo katika hii Dira mpya ili tuweze kuwa na kilimo cha kisasa kisichotegemea mvua”
Maadhimisho hayo ya Uhuru yamebeba kauli mbiu isemayo “Umoja na mshikamano ni chachu ya maendeleo ya taifa letu” kauli mbiu inayotilia mkazo umuhimu wa kuwa na umoja na mshikamano miongoni mwa wananchi wa taifa hilo katika juhudi za kuleta maendeleo endelevu.
Imeandaliwa na Amri Ramadhani Sauti ya Amerika Dar es Salaam.
Forum