Umoja wa Mataifa nchini DRC unafanya uchunguzi kuhusu madai ya rushwa ya ngono dhidi ya baadhi ya walinzi wa amani kutoka Tanzania walioko kaskazini-mashariki mwa DRC.
Taarifa ya Umoja wa Mataifa inasema wachunguzi wamepelekwa katika kijiji cha Mavivi ambako kuna dalili za awali za ngono na wasichana wadogo na vile vile madai kwamba wanajeshi hao wamezaa na wasichana walio chini ya umri wa miaka 18.
Taarifa hiyo ilisema kuwa serikali za Tanzania na DRC zimearifiwa kuhusu madai hayo, na kwamba hatua zitachukuliwa endapo madai hayo yatathibitishwa. Wanajeshi ambao inadaiwa walifanya vitendo hivyo hivi sasa wamebaki kambini kwao.
Umoja wa Mataifa pia umesema utatoa huduma za ushauri nasaha na missada mingine kwa wahanga wa vitendo hivyo.
Kwa miezi kadha Umoja wa Mataifa umekuwa ukikabiliwa na shutuma matumizi mabaya ya ngono yanayofanywa na walinzi wake wa amani katika nchi za Jamhuri ya Afrika ya Kati na DRC.
Jeshil la ulinzi wa amani DRC lina jumla ya wanajeshi elfu 20 kutoka nchi kadha na lilianza kazi hiyo mwaka 1999.