Sakati la madai ya ulaji rushwa wa zaidi ya shilingi bilioni 133 kwenye akaunti ya madeni ya nje yaani EPA katika Benki Kuu ya Tanzania, BOT, ilivuma mwaka 2008 ikihusisha baadhi ya vigogo wa benki hiyo, wafanya biashara maarufu pamoja na maafisa wa katika serikali kuu.
Serikali iliunda timu maalumu kuchunguza sakata hilo ambalo liliongozwa wakati huo na mwanasheria mkuu wa serikali, Johnson Mwanyika. Wajumbe wengine kwenye timu hiyo walikuwa mkurugenzi mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa-TAKUKURU, Dr. Edward Hosea na Inspekta mkuu wa polisi Said Mwema.
Shutuma kuu katika kashfa hii zilidai kuwa baadhi ya makampuni yaliyohusika yalidai kuwa yalipokea fedha kutoka akaunti hiyo kulipa madeni ambayo Tanzania ilikuwa ikidaiwa nje, lakini shutuma ni kwamba mengi ya madeni hayo yalikuwa tayari yamesamehewa.
Jumla ya kesi 14 za EPA zilifunguliwa kwa kishindo na mkurugenzi wa mashtaka-DPP, Dr. Eliezer Feleshi kufuatia kumalizika kwa uchunguzi wa tume ya rais. Ndani ya kesi hizo ilitolewa hukumu ya washukiwa wawili, Rajab Maranda na Farijala Hussein, ambao ni wana ndugu waliopatiwa kifungo cha miaka mitano kila mmoja.
Na mwishoni mwa mwezi Disemba washitakiwa wengine wawili ambao ni ndugu waliohusishwa katika madai haya ya ulaji rushwa wa EPA, Johnson Lukaza na Mwesigwa Lukaza waliachiwa huru na mahakama ya hakimu mkazi Kisutu, Dar Es Salaam baada ya kuonekana hawana hatia kwenye ubadhirifu huo.