Katika kampeni za uchaguzi mkuu wa Tanzania wagombea kutoka pande zote wamekuwa wakitoa ahadi chungu nzima katika jitihada ya kuvutia kura.
Mgombea urais kupitia umoja wa Ukawa, Edward Lowassa, anakampeni chini ya sera ya elimu, elimu, elimu, akiahidi, pamoja na mambo mengine, elimu bure kuanzia ngazi ya shule za msingi hadi chuo kikuu.
Kwa upande wake mgombea wa CCM, John Magufuli, anaahidi Tanzania ya viwanda, fedha taslimu za maendeleo kwa vijiji na mahakama za kupambana na ufisadi katika utawala wake endapo atachaguliwa.
Wachambuzi na wananchi wengi wanajiuliza endapo haya yote yanawezekana, yatagharimu kiasi gani cha fedha na zitatoka wapi. Wagombea hawaelezi kinagaubaga watagharamia vipi ahadi hizo.
Katika mfululizo wa makala haya maalum VOA imezungumza na wataalam na kuuliza swali la msingi - je ahadi hizi zinaweza kutekelezeka?