Wanaharakati wanaofuatilia mazungumzo ya amani ya Sudan Kusini wanaeleza wasi wasi wao kuhusu kupatikana suluhisho la kudumu kwa mzozo wa nchi hiyo kukiwa zimebaki chini ya saa 24 kabla ya muda wa mazungumzo kumalizika huko Addis Ababa nchini Ethiopia.
Muungano wa wanaharakati wa asasi za kiraia unaojulikana kama “Jopo la kufufua Amani” ulitoa taarifa Alhamis ikiviomba vyama vinavyopingana kuweka pembeni maslahi yao binafsi na ya kisiasa na kuchukua hatua za dhati na za kuaminika ili kuhakikisha mafanikio kwenye mashauriano ya wiki mbili kuhusu namna ya kumaliza ghasia huko Sudan Kusini.
Taarifa ilieleza kwamba “hii leo nchi yao ipo kwenye njia panda na mamilioni ya raia kwa mara nyingine wanawategemea viongozi wao. Wanategemea kwamba maamuzi ya kizalendo yatakaochukuliwa hii leo huko Addis Ababa ndio yataokoa maisha ya binadam, kurejesha heshima ya wanawake na watoto na kutoa fursa kwa vijana kutimiza ndoto zao”.
Kipengele cha saba cha pendekezo juu ya kufufua serikali ya mpito ya umoja wa kitaifa inapendekeza kuwepo na makamu rais wanne katika kipindi cha miezi 36 ya mpito ya kusimamia utekelezwaji wa mageuzi ulioelezea kurejesha tena mkataba wa amani uliovunjika mwaka 2015.
Rajab Mohandis ambaye anawakilisha kundi la jamii ya kiraia kwenye mazungumzo hayo alisema viongozi wa vyama vinavyopingana wanapendelea kushika nyadhifa. Aliendelea kusema kwamba wamewaeleza mara kwa mara viongozi hao kwamba mazungumzo yanatakiwa kulenga maslahi ya watu na sio kulenga kwenye madaraka.