Mitaa katika mji mkuu wa Sudan ilikuwa mitupu Alhamisi wakati upinzani wa kiraia ukijiandaa kuadhimisha kumbukumbu muhimu katika mapambano ya miongo kadhaa dhidi ya utawala wa kijeshi kwa kufanya maandamano mapya dhidi ya majenerali.
Wakitarajia maandamano mamlaka ilitangaza kwamba Alhamisi hakuna kazi na walioshuhudia walisema waliona kundi kubwa la jeshi katika mitaa ya Khartoum tangu Jumatano. Wanajeshi pia walifunga madaraja ya mto Nile yanayounganisha Khartoum na viunga vyake, Omdurman na Khartoum Kaskazini, mashuhuda wamesema.
Aprili 6 ni tarehe muhimu kwa upinzani wa kiraia nchini Sudan ukiadhimisha kumbukumbu ya maandamano ya mwaka 1985 na mwaka 2019 ambayo yaliishia kuwaondoa madarakani viongozi wawili waliokuwa wamechukua madaraka kwa njia ya mapinduzi.