Waziri wa sheria wa Sudan Awad Hassan Elnour amekanusha madai yaliyotolewa na watu waliokoseshwa makazi katika eneo la Jebel Marra huko Dafur kuwa wameathiriwa na kemikali zilizotumiwa na serikali.
Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International liliripoti alhamisi kuwa tangu mwezi Januari wakazi wa Jebel Marra wameripoti kupata malengelenge, muasho, ngozi kuchubuka, matatizo ya macho ikiwemo kupoteza kabisa nguvu ya kuona, kutapika damu, kuharisha na matatizo ya kupumua.
Amnesty imedai matatizo hayo ni kuotokana na silaha za kemikali zilizotumiwa na Serikali. Takriban watu 250 wakiwemo watoto huenda wamekufa kutokana na shambulizi la kemikali huku ikikisiwa kuwa mamia wengine wameathirika.
Hata hivyo waziri Awad Hassan kwenye barua alioandika Alhamisi amesema kuwa maafisa wa Serikali wameshangazwa na madai hayo.