Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Machi 29, 2024 Local time: 01:32

Somalia yapeleka balozi Afrika Kusini


 Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud
Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud
Kwa mara ya kwanza Somalia imepeleka balozi wake Afrika Kusini, taifa lenye uchumi mkubwa barani Afrika. Balozi mpya Sayid Sheriff anasema ana matumaini makuu anapopandisha bendera ya kidiplomasia ya Somalia baada ya miongo mingi ya kutokuwa na uthabiti wa kisiasa. Anasema anapanga kuwafikia maelfu ya raia wa Somalia waliokimbilia Afrika Kusini.

Sayid Sheriff ni balozi wa kwanza wa Somalia kupelekwa Afrika Kusini.Na kama ilivyo kawaida kwa mabalozi wanaokwenda nchini humo, alipokelewa kwa shangwe na kuandaliwa sherehe maalum. Somalia haijawa na serikali thabiti kwa miongo mingi. Ni taifa ambalo limekumbwa na ukame na njaa; vita vya wenyewe kwa wenyewe, wanamgambo wa al-Shabab wenye ushirika na mtandao wa kigaidi wa al-Qaida na tatizo la uharamia.

Akimkaribisha balozi huyo nchini humo rais Jacob Zuma alisema; “Kutaabika kwao kutokana na ukame na njaa, na njia waliofikia katika kukarabati taifa lao ni njia tuliyopitia. Tutasimama nao kidete na kuwasaidia katika ujenzi mpya wa taifa lao.” Bwana Zuma amesema Afrika Kusini itatoa dola milioni 11 kusaidia ujenzi mpya wa Somalia katika miundo mbinu na taasisi zake.

Akizungumza na sauti ya Amerika, balozi Sheriff alisema taifa lake na Afrika Kusini zina mahusiano ya muda mrefu. Alisema zama zile Somalia ilisaidia chama cha African National Congress kupigana dhidi ya serikali ya ubaguzi wa rangi. Lakini wakati Afrika Kusini ilipopata uthabiti wa kidemokrasia mwaka wa 1994, Somalia ilikuwa imetumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Balozi huyo alionya kuwa mabadiliko Somalia hayatakuwa ya haraka akiashiria mlipuko wa bomu uliotekelezwa na mhanga wa kujitolea Jumanne karibu na kasri ya rais. Alisema baada ya vita vya zaidi ya miaka 21 vya wenyewe kwa wenyewe mabadiliko hayawezi kuonekana mara moja. Amani haitajitokeza kama muujiza, lakini Somalia inaanza kushuhudia amani hatua kwa hatua.
XS
SM
MD
LG