Uchaguzi wa Rais wa Marekani kwa sasa uko kwenye darubini ya ulimwengu lakini huko pembe ya Afrika, harakati za uchaguzi zinaendelea kwa ajili ya uchaguzi wa Somalia, ambao unatarajiwa mwisho wa mwezi Novemba, ambao utajumuisha uchaguzi wa Rais pamoja na wabunge wa mabaraza mawili.
Mbunge wa Somalia, Abdiweli Qanyare amesema kwa ujumla maandalizi ya uchaguzi huo yanaendelea vyema. Anasema kufikia sasa hawajapata malalamiko yoyote ijapokuwa kila uchaguzi unapofanyika hakukosi wale wanaolalamika kuwa sio wa haki.
Mwakilishi maalum wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa Somalia Michael Keating amesema kuna changamoto za kiusalama katika kuandaa uchaguzi huo kutokana na mapigano ya zaidi ya miongo mitatu na ukosefu wa sheria pamoja na tishio kutoka kundi la kigaidi la al Shaabab.