Milipuko na mashambulizi ya bunduki katika mgawaha mmoja mashuhuri karibu na eneo la pwani la mji mkuu wa Somalia, Mogadishu yameuwa watu wasiopungua watatu, na wengine wanne kujeruhiwa.
Milipuko hiyo ilitokea katika mgahawa wa Lido Sea Food majira ya sala ya magharibi, na kufuatiwa na mashambulizi ya bunduki baina ya walinzi wa hoteli hiyo na washambuliaji waliokuwa wakijaribu kuingia ndani.
Mohamud Hared, mmiliki wa hoteli nyingine ya karibu aliiambia VOA kuwa walisikia milio ya bunduki na baadaye milipuko miwili ilifuatia.
Mwandishi wa habari mmoja ndani ya hoteli iliyoshambuliwa aliambia VOA kuwa yeye pamoja na watu wengine 20 walibanwa ndani ya hoteli hiyo wakati mashambulizi yakiendelea.
Ripoti za awali zilisema vikosi vya usalama vya serikali haraka vilizingira hoteli hiyo na mitaa ya jirani.