Marekani na Umoja wa Mataifa wametangaza kuwa Israel na Hamas wamekubaliana juu ya sitisho la mapigano la kibinadamu kwa saa 72 bila masharti.
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry anasema sitisho hilo la mapigano litaanza saa mbili asubuhi leo Ijumaa kwa saa za huko Mashariki ya Kati na litatumiwa kuwapa raia wa Gaza ahueni kutokana na ghasia hizo.
Raia pia wataweza kuzika jamaa zao waliouawa katika mapigano hayo, kununua vyakula na kukarabati majengo yaliyoharibiwa.
Mara baada ya sitisho hilo la mapigano kuanza,wajumbe wa Israel na Palestina watakwenda Cairo kwa mazungumzo juu ya kuongeza muda wa kusitisha vita hivyo.