Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Aprili 23, 2024 Local time: 09:58

Shambulizi la kigaidi lauwa 68 Nairobi


Baadhi ya watu waliovamiwa na magaidi katika maduka ya Westgate Mall, Nairobi Septemba 21, 2013
Baadhi ya watu waliovamiwa na magaidi katika maduka ya Westgate Mall, Nairobi Septemba 21, 2013
Kenya inaomboleza vifo vya watu 68 waliouawa katika shambulizi la kigaidi katika maduka ya kifahari ya Westgate Mall, nje kidogo ya jiji kuu la Nairobi.

Jumapili jioni rais wa Kenya Uhuru Kenyatta aliwahutubia wakenya na kuwasihi wawe watulivu wakati operesheni zinaendelea kukomboa mateka ambao bado wameshikiliwa na magaidi katika Westgate Mall.

Mwandishi wa idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Amerika Mwai Gikonyo, anaripoti kuwa zaidi ya watu elfu moja wameokolewa na 175 wamelazwa katika hospitali mbalimbali za Nairobi. Anasema kikosi maalum cha Israel Mossad, pia kinasaidiana na wanajeshi wa Kenya kukomboa mateka walionaswa na magaidi ndani ya maduka hayo.

Shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya linaendelea kutoa huduma muhimu kwa waathiriwa wa shambulizi hilo.Na Serikali imewaomba wananchi wasiende karibu na maduka hayo wakati msako huo unapoendelea.

Akizungumza na Sauti ya Amerika, Katibu wa mawasiliano, Kenya bw. Ezekiel Mutua alisema wakenya wameonyesha mshikamano na umoja wakati wa msiba huu mkubwa wa taifa. Alisema wengi wamepanga foleni tangu Jumamosi kutoa damu kusaidia kuokoa maisha ya walionusurika.

Kundi la wanamgambo la al-Shabab kutoka Somalia ambalo lina ushirika na mtandao wa kigaidi wa al-Qaida limedai kutekeleza mashambulizi hayo.

Rais wa Kenya, bw. Kenyatta ambaye amempoteza mpwa wake katika shambulizi hilo amesema magaidi hao watasakwa na kuadhibiwa vikali. Amesema Kenya itaendelea kupambana dhidi ya ugaidi na kushukuru mataifa ya Afrika na nje ya bara hilo kwa msaada wao kwa Kenya wakati wa msiba huu mkubwa nchini humo.

Aidha bw. Kenyatta alisistiza kuwa huu sio wakati wa kutoa ilani kwa wageni kutotembelea Kenya kwani kufanya hivyo ni kulidhoofisha taifa hilo zaidi wakati dunia inapotakiwa kuonyesha umoja na ujasiri kukabiliana na tatizo la ugaidi.

Taarifa zaidi zinasema rais wa Marekani Barack Obama amezungumza kwa njia ya simu na rais Kenyatta, huku wizara ya ulinzi ya Marekani ikisema ipo tayari kutoa msaada kwa Kenya.

Hili ni shambulizi la pili lenye maafa makubwa nchini Kenya tangu magaidi waliposhambulia taifa hilo la Afrika Mashariki Agosti 7, 1998 ambapo zaidi ya watu 200 waliuawa.
XS
SM
MD
LG