Maafisa nchini Ufaransa wanasema mshambuliaji aliyekuwa amejihami kwa kisu aliwajeruhi watu sita Jumatano asubuhi katika kituo cha treni chenye shughuli nyingi mjini Paris.
Waziri wa mambo ya ndani wa Ufaransa, Gerald Darmanin amewaambia waandishi wa habari kwamba polisi walimpiga risasi mshambuliaji huyo ambaye alikuwa kwenye hali ya "kati ya maisha na kifo" baada ya kupelekwa hospitali.
Shambulio hilo lilitokea katika kituo cha treni cha Gare du Nord, moja ya eneo lenye shughuli nyingi zaidi barani Ulaya.
Sababu ya shambulizi hilo haijulikani na mamlaka zinasema zimeanzisha uchunguzi wa uhalifu kwa tukio hilo.