Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Julai 23, 2024 Local time: 17:18

Shambulizi jingine la kujitoa mhanga lafanyika Nigeria


Shambulizi la kujitoa mhanga katika soko moja huko nchini Nigeria
Shambulizi la kujitoa mhanga katika soko moja huko nchini Nigeria

Ripoti kutoka mji wa Maiduguri kaskazini mashariki mwa Nigeria zilisema watu wasiopungua watano wamefariki baada ya mlipuaji bomu wakujitoa mhanga kujilipua katika soko la Gamboru hapo Ijumaa.

Walioshuhudia shambulizi hilo la Ijumaa walisema watu kadhaa pia walijeruhiwa. Japokuwa hakuna mtu yeyote aliyedai kuhusika na shambulizi hilo lakini eneo hilo ni kiini cha harakati za kundi la Boko Haram. Kundi hilo limefanya mfululizo wa mashambulizi katika eneo hilo matukio ambayo yaliuwa watu kadhaa katika wiki za karibuni.

Jeshi la Nigeria
Jeshi la Nigeria

Hapo Alhamis jeshi la Nigeria lilisema kwamba liliwaokoa wanawake, watoto na wanaume wazee 59 waliokuwa wameshikiliwa mateka na wanamgambo wa ki-Islam wa kundi la Boko haram.

Maafisa wa jeshi walisema wanajeshi walivamia maficho ya Boko Haram karibu na Maiduguri. Maafisa walisema magaidi wengi waliuwawa na pia walikamata idadi kadhaa ya silaha na magari.

Msemaji wa jeshi, Kanali Sani Kukasheka Usman aliiambia Sauti ya Amerika-VOA kwamba “popote pale kwenye mafanikio ya aina hii, inasaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza ari siyo tu majeshi yaliyo katika mapambano, lakini kwa wanigeria wote kwa jumla”.

Mateka waliookolewa ni pamoja na wanaume wazee watano pamoja na wanawake na watoto 54. Baadhi ya mateka walioachiliwa waliwaeleza waandishi wa habari kwamba magaidi waliwapatia chakula kidogo na mara kwa mara waliwatishia kuwauwa.

Wanamgambo wa Boko Haram mara kwa mara walishambulia vijiji na kuwateka wakazi pamoja na kuwalazimisha kubadili dini na kuingia katika uislam.

Wanamgambo wa Boko Haram
Wanamgambo wa Boko Haram

Kundi la Boko Haram lilishambulia shule moja na kuwateka nyara wasichana wa shule takribani 300 kutoka mji mdogo huko kaskazini-mashariki mwa Nigeria mwaka jana, tukio ambalo linalaaniwa na dunia nzima. Zaidi ya wasichana 200 bado wamepotea.

Boko Haram limekuwa likifanya kampeni za ugaidi za umwagaji damu kwa lengo lake la kuigeuza Nigeria kuwa katika nchi inayofuata uislam wenye siasa kali.

XS
SM
MD
LG