Waziri Sy aliyetembelea eneo shambulio lilitokea katika jimbo la mashariki ya mji mkuu wa Wagadougou anasema maafisa wa uokozi wangali wanawatafuta wachimba migodi wengine ambao bado hawajulikani walipo.
Kampuni ya Canada ya Semafo inayosimamia kazi za mgodi huo imeeleza Ijumaa kwamba mabasi yake matano yaliyo kuwa yanawasafirisha wafanyakazi kuelekea kazini yalishambuliwa na wanamgambo wasiojulikana wa makundi ya wafuasi wa itikadi kali za Kiislamu yanayoendesha shughuli zake kaskazini na mashariki ya Burkina Faso.
Taifa hilo la Afrika Magharibi linalofahamika kwa utulivu wake limekuwa likipambana na mashambulizi ya kigaidi yaliyowasababisha maelfu ya watu kukimbia makazi yao tangu mwanzoni mwa mwaka huu kulingana na mashirika ya kimataifa ya huduma za dharura.