Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Machi 02, 2024 Local time: 04:27

Serikali ya Burundi yaakhirisha uchaguzi wa rais


Mivutano ya kisiasa Burundi inafuatia hatua ya rais kutaka kuongeza muhula mwingine madarakani
Mivutano ya kisiasa Burundi inafuatia hatua ya rais kutaka kuongeza muhula mwingine madarakani

Burundi inachelewesha uchaguzi wake wa rais kufuatia maandamano dhidi ya azma ya rais kutaka kuwania muhula wa tatu madarakani. Hatua hiyo imekuja wakati taasisi za kieneo zikisihi kuendeleaza mashauriano na upinzani ili kutatua mgogoro wa kisiasa nchini humo.

Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza alitangaza uamuzi huo Jumanne jioni wa kuakhirisha upigaji kura wa rais hadi Julai 15 kiasi cha wiki mbili zaidi na tarehe iliyopangwa awali.

Ghasia za wananchi wakipinga rais kuwania muhula wa tatu madarakani
Ghasia za wananchi wakipinga rais kuwania muhula wa tatu madarakani

Uchaguzi wa wabunge pia umesogezwa mbele kiasi cha mwezi mmoja na hivi sasa umepangwa kufanyika Juni 29.

Msemaji wa rais, Gervais Abayeho aliiambia Sauti ya Amerika-VOA kwamba ratiba mpya imepangwa ili kutoa muda kwa upinzani kujipanga kwa ajili ya upigaji kura. “Hivyo vyama vya upinzani ambavyo vilikuwa vinalalamika havikuwa na muda wa kutosha kufanya kampeni hilo limeshughulikiwa, hivyo basi wanaweza kutumia muda huu kufanya hivyo”.

Vyama vya upinzani na wanaharakati wa makundi ya kiraia waliongoza wiki kadhaa za maandamano ya mitaani dhidi ya mpango wa Rais Nkurunziza wa kuwania muhula wa tatu madarakani ambapo upinzani unasema ni kinyume cha sheria.

Baadhi ya viongozi wa upinzani wameikataa ratiba mpya ya uchaguzi ilipopendekezwa mara ya kwanza na tume ya uchaguzi nchini humo.

Msemaji wa ushirika wa upinzani aliiambia Sauti ya Amerika-VOA hapo Jumanne kwamba tume haina mamlaka ya kisheria kubadilisha tarehe ya uchaguzi.

Ucheleweshaji wa uchaguzi unafuatia mapendekezo yaliyowasilishwa mwezi uliopita na wakuu wa nchi wanachama wa jumuiya ya Afrika mashariki-EAC.

Ghasia za kisiasa Burundi
Ghasia za kisiasa Burundi

Wakati huo huo, mkutano wa kimataifa kwa eneo la maziwa makuu unaisihi serikali kuendelea na mashauriano ya kitaifa na wanachama wa upinzani pamoja na makundi ya kiraia ili kubuni njia ya kumaliza mgogoro huu wa sasa.

Ambeyi Ligabo ni mkurugenzi wa utawala na demokrasia katika ICGLR.“Tuna matumaini kwamba pande zote zinaweza kuona umuhimu wa kuwa na mashauriano ili kuepuka ghasia zozote na pia kuvuruga harakati za kiuchumi na biashara miongoni mwa nchi wanachama wa ICGLR”.

Umoja wa Mataifa ulielezea wasi wasi kuhusu kusambaa kwa ghasia za kisiasa wakati wa upigaji kura.

Jumanne, kamishna mkuu wa haki za binadamu, Zeid Ra’ad Al Hussein alisema Umoja wa Mataifa umekuwa ukipokea habari za kutia wasi wasi mkubwa kuhusu mauaji, utekaji nyara na vitendo vingine vya ghasia vilivyofanywa na wanamgambo wanaoiunga serikali.

XS
SM
MD
LG