Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Desemba 09, 2023 Local time: 11:00

Senegal yaitoa Afrika kimasomaso


Wachezaji wa Senegal wakishangilia mbele ya mashabiki wake baada ya mchezo kumalizika mjini Moscow, Russia, Jumanne, Juni 19 2018.
Wachezaji wa Senegal wakishangilia mbele ya mashabiki wake baada ya mchezo kumalizika mjini Moscow, Russia, Jumanne, Juni 19 2018.

Timu ya taifa ya Senegal imekuwa timu ya kwanza ya Afrika kupata ushindi katika Kombe la Dunia Russia 2018 linaloendelea nchini Russia, kwa kuifunga Poland magoli (2 – 1).

Senegal ambayo ipo kundi H, imejiweka katika nafasi nzuri ya kusonga mbele na kuingia raundi ya pili na mtoano kwa kuwa sasa imejipatia pointi 3, sawa na Japan ambayo nayo imepata ushindi kama wa Senegal, kwa kushinda (2 – 1) dhidi ya Colombia.

Nahodha wa Senegal, Sadio Mane akishangilia mara baada ya mchezo kumalizika.
Nahodha wa Senegal, Sadio Mane akishangilia mara baada ya mchezo kumalizika.

Goli la kwanza la Senegal limetokana na kujifunga kwa Thiago Cionek mchezaji wa Poland, baada ya kombora kupigwa na kiungo wa Senegal, Idrissa Gueye katika dakika ya 37 ya kipindi cha kwanza.

Goli la pili la Senegal limefungwa na M’Baye Niang katika dakika ya 60, baada ya kukimbia kutoka nje ya uwanja alipokuwa akitazamwa baada ya kuumia. Niang aliuwahi mpira uliokuwa ukirudishwa kwa kipa wa Poland, Wojciech Szczesny, na kujikuta akiwa peke yake na nyavu na kuuzamisha mpira.

Kabla ya dakika chache mchezo kumalizika, Grzegorz Krychowiak wa Poland, alifunga goli na kuyafanya matokeo ya mchezo huo kuwa wa (2 -1) katika dakika ya 86.

Senegal ambayo inashiriki michuano hii kwa mara ya pili, itapambana na Japan, Jumapili ya tarehe 24 mwezi huu na endapo ikishinda mchezo huo, itajihakikishia kucheza raundi ya pili ya Kombe la Dunia Russia 2018.

XS
SM
MD
LG