Rufaa hiyo ilihusu suala la kuwataka wanawake walio na viwango vya juu vya homoni za kiume, maarufu testosterone, kupunguza viwango hivyo kwa kutumia dawa.
Bingwa wa mara mbili wa mbio za mita 800 za Olimpiki, Caster Semenya, Jumanne alishinda kesi katika Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu, alikowasilisha rufaa akidai haki zake zimekiukwa, katika suala la kuwataka wanawake walio na viwango vya juu vya homoni za kiume, maarufu testosterone, kupunguza viwango hivyo kwa kutumia dawa.
Semenya, raia wa Afrika Kusini, mwenye umri wa miaka 32, ambaye anaorodheshwa kama "tofauti katika ukuaji wa kijinsia", amekataa kutumia dawa za kupunguza homoni hizo, kama ilivyoamrishwa na shirikisho la kimataifa la riadha, World Athletics, ikiwa anataka kushiriki katika mbio za umbali aliouchagua.
Semenya alishindwa katika rufaa yake katika Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo, na mahakama ya rufaa ya Uswizi ilithibitisha uamuzi wa mahakama ya juu ya michezo.
Aliwasilisha kesi dhidi ya Uswizi kama sehemu ya mapambano ya kisheria ya muda mrefu. Katika uamuzi wake, ECHR yenye makao yake mjini Strasbourg "iligundua haswa kwamba Semenya alikuwa hajapewa ulinzi wa kutosha wa kitaasisi na kiutaratibu nchini Uswizi, ili kuwezesha malalamiko yake kuchunguzwa ipasavyo".
Ushindi wa mchezaji huyo kwa kiasi kikubwa ni wa ishara tu, kwani hautilii shaka uamuzi wa shirika la World Athletics na haumfungulii njia Semenya kurejea katika mashindano ya mbio za mita 800.
Semenya alishinda medali ya dhahabu katika Michezo ya olimpiki ya London mwaka 2012, na ya mjini Rio De Jenairo, mnamo mwaka 2016.
Forum